MAANDALIZI ya mbio zinazofanyika ndani ya Pori la Akiba la Pande (Pande Marathon) msimu wa pili, yamekamilika na atakayeshindwa kufanya usajili wake leo, imekula kwake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mbio hizo za msimu wa pili, zinatarajiwa kufanyika Agosti Mosi mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angel Kairuki.
Mbali ya Waziri Kairuki baadhi ya wageni maalum waliothibitisha kushiriki ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, Waziri na Mbunge wa zamani, Dk. Khamis Kingwang’ala na wengine.
Mbio hizo zinazoandaliwa na Taasisi ya Kukuza Michezo ya Msakuzi Sports Promotion, msimu huu wa pili zitakuwa za aina yake kwani zinatarajia kushirikisha zaidi ya watu 1000 kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi huku zikibeba kauli mbiu ya ‘Afya na Utalii’.
Akizungumzia Maandalizi ya Mbio hizo, Mwenyekiti wa Msakuzi Sports Promotion Dk. John Kisimbi, amesema usajili unaendelea kwa kasi na maandalizi yamekamilika na kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa.
“Tunawashukuru sana wadau wetu wote, mwitikio wa kujisajili umekuwa mkubwa na tumebaki na siku moja tu. Bado kuna nafasi ya kufanya usajili, muhimu siku ya Jumamosi tukutane Pande, tukafurahi pamoja,” anasema Dk. Kisimbi.
Aliishukuru Mamlaka ya Usimamizi ya Wanyama Pori Tanzania (TAWA) kwa ushirikiano wao kwani wamekuwa wakifanya kila linalowezekana kuhakikisha mbio hizo zinafanikiwa.
Amesema msimu wa pili utakuwa wa aina yake kwani mambo mengi yameboreshwa hivyo wananchi wasipange kukosa.
“Niwahakikishie washiriki wetu na wananchi kwa ujumla. Safari hii usipange kukosa mambo mengi yameboreshwa na hakika tutakuwa na siku nzuri sana,” alisisitiza.
“Pande Marathon ni mbio za aina yake na za kipekee sana, washiriki watakimbia huku wakifurahia vifutio vya utalii wa wanyama wa aina mbalimbali na uoto wa asili ambao huongeza mvuto na hamasa kwa wakimbiaji. Hii usipange kukosa kabisa,” alisema Dk. Kisimbi.
Tofauti na mbio zingine, Dk. Kisimbi anasema washiriki mbali ya kukimbia na kujenga afya, pili wanafanya utalii na tatu washindi wataibuka na zawadi nono.

“Msimu wa kwanza mwaka jana, tulifanikiwa sana, washiriki zaidi ya 500 walijitokeza na baada ya mbio walipata burudani mbalimbali kama vile live bendi, nyama choma za pori, walipata fursa ya kuangalia wanyama na hakuna aliyetaka kuondoka, safari hii mambo ni moto zaidi.
Kwa upande wake, Mratibu wa mbio hizo, Filbert Mosha amesisitiza kuwa siku ya Marathon Agosti Mosi baada ya mbio kutakuwa na mambo mengi ambayo hayajapata kutokea kwenye marathon yoyote nchini.
“Burudani za bendi kubwa na maalum za muziki, wasanii mbalimbali na watu maarufu watakuwepo. Vinywaji vya aina zote, nyama choma za pori, kuku na aina zingine zote zitakuwepo. Siku kama hiyo inakosaje,?” alisisitiza Mosha.
Amewakumbusha wanaoendelea kujisajili kwamba usajili unafanyika kidigitali kupitia tovuti www.pandemarathon.store.tz.