WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amewashangaa wanaojitokeza kutetea watuhumiwa waliokamatwa na jeshi la polisi akiwemo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Melikisedeki Kaijage akisisitiza kuwa hakuna mtu wala taasisi inayolengwa kwa uonevu.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Waziri Katambi ametoa ufafanuzi huo leo 29 Julai 2026, visiwani Zanzibar, kufuatia kuwepo kwa malalamiko nchini baada ya jeshi la polisi kuwakamata watuhumiwa 130 wa makosa mbalimbali, hatua iliyoibua mijadala na utetezi kutoka kwa baadhi ya wananchi na makundi ya kijamii.
Akifafanua suala hilo, Katambi ameeleza kuwa kama ingekuwa Serikali ina lengo la kuwalenga wanataaluma au taasisi fulani, wataalamu wengi wasingekuwa huru nchini kama walivyo sasa, hivyo akawataka wananchi kuacha kutetea mambo ambayo hawana uelewa nayo wala ushahidi nayo.
Aidha, Waziri huyo ametoa onyo kwa jamii kuacha kuhoji au kuingilia mashauri ambayo tayari yamo mahakamani, akibainisha kuwa mfumo wa sheria lazima uachwe ufanye kazi yake kwa uhuru na uwazi bila shinikizo la kisiasa au la kijamii.
“Hakuna mtu ambaye anaweza kulengwa wala hakuna kusudio lolote linalokusudia kumlenga mtu au taasisi na kama ingekuwa kuna lengo maalumu mbona kuna wanataaluma wengi wako huru, kwa hiyo tusitetee vitu ambavyo hatuvijui na hasa kwenye mashauri ambayo yako mahakamani kwa sasa hatuna ujasiri wa kuyahoji,” alisema Katambi.
Akihitimisha maelezo yake, Katambi amesisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na katiba bila kumwogopa mtu yeyote, huku akihakikisha kuwa kila mtuhumiwa atapewa haki yake stahiki kupitia vyombo vya sheria.