Tundu Lissu akiwa mahakamani
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa wito kwa Mkuu wa Gereza la Ukonga kuhakikisha usalama wa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kufuatia taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza hofu kuhusu hali yake akiwa gerezani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Katika taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia, chama hicho kimesema kimepokea kwa masikitiko na wasiwasi taarifa ya World Liberty Congress, shirika linalojihusisha na utetezi wa demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria na uhuru wa kisiasa duniani, ambayo imeeleza hofu kuhusu usalama wa Tundu Lissu.
Chadema kimemtaka Mkuu wa Gereza la Ukonga kutoa taarifa kuhusu hali ya Mwenyekiti wake na kuhakikisha usalama wake pamoja na kuheshimiwa kikamilifu kwa haki zake za kikatiba na kibinadamu akiwa chini ya ulinzi wa mamlaka za magereza.
Aidha, chama hicho kimetoa wito kwa jumuiya za kimataifa, taasisi za kidemokrasia na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya Tundu Lissu na kutumia njia za kidiplomasia na kisheria zilizopo ili kuhakikisha haki zake zinalindwa na kuheshimiwa kwa mujibu wa sheria.
Taarifa ya Chadema imekuja kufuatia mjadala ulioibuka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu usalama wa Tundu Lissu akiwa gerezani.