ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, amehoji kauli ya Makamu wa Rais, Balozi Emmanuel Nchimbi, aliyewataka Watanzania kupambana ili kupata Katiba Mpya, akisema ikiwa Rais Samia Suluhu Hassan ana nia ya dhati ya kuipata Katiba hiyo, hakuna sababu ya wananchi kuambiwa waipambanie.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza katika mahojiano na Saut Digital, Ijumaa 24 Julai 2026, Askofu Bagonza alisema kauli ya Makamu wa Rais imeibua maswali muhimu kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.
Alisema kama kweli hitaji la Katiba Mpya ni msimamo wa Rais, kama alivyosema Makamu wa Rais, basi haieleweki kwa nini wananchi wanapaswa kupambana ili kuipata.
“Makamu amesema Rais anaitaka kwa sababu iliwekwa kwenye ilani. Swali langu ni, kama Rais anaitaka kwa nini tuipambanie? Tunapambana na nani ili kuipata? Na kama Rais anaitaka kweli, kwa nini hasemi mwenyewe badala ya kusemewa?” alihoji Askofu Bagonza.
Kwa mujibu wa Bagonza, kauli ya Makamu wa Rais ni ishara nzuri ya kutambua umuhimu wa Katiba Mpya, lakini viongozi wakuu wa Serikali wanapaswa kutoa msimamo wao wazi ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi.

Awali, akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), uliofanyika 24 Julai jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais Emmanuel Nchimbi aliwataka Watanzania kuongeza juhudi za kupigania Katiba Mpya yenye maridhiano ya wadau wote.
“Nikiambiwa kuna jambo moja la kuwaambia Watanzania, nitasema pambaneni mpate Katiba Mpya; katiba ambayo ina makubaliano ya wadau wote, katiba yenye muafaka katika taifa na ambayo kila Mtanzania atajivunia,” alisema Nchimbi.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa wakati wa maandalizi ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025, pamoja na mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa mwaka 2025, wananchi wengi wameonyesha hitaji la kupatikana kwa Katiba Mpya.
Balozi Nchimbi alisema mapendekezo yaliyopo yanaelekeza mchakato wa Katiba Mpya ukamilike ifikapo mwaka 2028 ili iweze kutumika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2029.