ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk. Ayub Rioba Chacha, ametoa tahadhari kuhusu umuhimu wa kulinda uhuru wa mawazo na fikra huru katika taasisi za elimu ya juu, kufuatia sakata la kisheria linalomkabili mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kaijage.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kauli ya Dk. Rioba imekuja wakati shauri linalomhusu Kaijage likiendelea kufuatiliwa na wadau mbalimbali wa haki za binadamu, wanazuoni na wananchi, hasa baada ya mhadhiri huyo kukabiliwa na mashtaka ya ugaidi.
Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Dk. Rioba amesema kuwa licha ya kutokuwa na taarifa za kina kuhusu maudhui ya tuhuma zinazomkabili Kaijage, taifa halipaswi kufikia hatua ya kujenga mazingira ya hofu yanayoweza kuzuia uhuru wa kufikiri, kuhoji na kukosoa.
“Sina uhakika na aina ya maudhui ya mhadhiri wa UDOM anayetuhumiwa kwa ‘ugaidi’, lakini ninashawishika kusema, kama Taifa, tusijiruhusu kufika huko! Tutakuwa Taifa la watu wajinga sana tukifika pahala tukadhani uhuru wa kufikiri, kuhoji na kukosoa unamilikiwa na watu fulani!” ameandika Dk. Rioba.
Amesisitiza kuwa jukumu la msingi la vyuo vikuu ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa kina na kufanya uchambuzi wa masuala mbalimbali kwa misingi ya kitaaluma.
Kwa mujibu wake, mazingira ya elimu ya juu yanapaswa kulinda uhuru wa mawazo huku yakihimiza mijadala yenye tija kwa maendeleo ya jamii.
Hata hivyo, Dk. Rioba amesema kuwa wanazuoni nao wana wajibu wa kuhakikisha uchambuzi na taarifa wanazozitoa zinafanywa kwa misingi ya taaluma na uwajibikaji, badala ya kuendeshwa kwa mfumo wa harakati zisizozingatia tafakuri sahihi.
Akihitimisha ujumbe wake, Dk. Rioba amesema haungi mkono jitihada zozote zinazoweza kufifisha uhuru wa mawazo au maoni, akisisitiza kuwa uhuru huo ni nguzo muhimu ya demokrasia, hususan ndani ya vyuo vikuu.
Kaijage alikamatwa 8 Julai 2026, kufuatia tuhuma zilizohusishwa na uchochezi wa maandamano ya umma yaliyofanyika 7 Julai 2026, kabla ya baadaye kukabiliwa na mashtaka ya ugaidi.
Shauri hilo linaendelea katika vyombo vya sheria, ambapo hatima ya tuhuma zinazomkabili itaamuliwa na mahakama kwa kuzingatia ushahidi utakaowasilishwa.