MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, amesema kuwa serikali haina sababu ya kusita kuridhia mkataba unaolinda watetezi wa haki za binadamu, akieleza kuwa hatua hiyo itaonesha dhamira ya taifa katika kulinda haki za msingi za wananchi.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Nchimbi amesema kuwa pale watetezi wa haki za binadamu wanapoanza kujenga hoja kuhusu usalama wa watu wanaowatetea, huwa ni dalili kwamba kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi na mamlaka husika.
“Tutakuwa serikali ya ajabu sana kama tutakataa kuridhia mkataba unaowalinda watetezi wa haki za binadamu,” amesema Nchimbi
Aidha, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kulinda amani na usalama wa wananchi, akisisitiza kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi katika mazingira salama.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), uliofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam, leo 24 Julai 2026.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na watetezi wa haki za binadamu ni muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria, kulinda haki za wananchi na kudumisha amani nchini.