WABUNGE nchini Ufaransa wanatarajiwa kupitisha sheria mpya itakayowazuia watoto walio chini ya umri wa miaka 15 kutumia mitandao ya kijamii, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi wa watoto dhidi ya athari zinazotokana na matumizi ya majukwaa ya kidijitali.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Endapo sheria hiyo itapitishwa, Ufaransa itakuwa nchi ya kwanza ndani ya Umoja wa Ulaya kuweka kikomo rasmi cha umri wa matumizi ya mitandao ya kijamii.Sheria hiyo inaungwa mkono na Rais Emmanuel Macron, ambaye ameifanya kuwa moja ya ajenda muhimu za kipindi chake cha mwisho madarakani.
Mpango uliowekwa unaonesha kuwa kuanzia 1 Septemba mwaka huu, watoto walio chini ya miaka 15 hawataruhusiwa kufungua akaunti mpya kwenye mitandao ya kijamii, huku akaunti zilizopo tayari zikitarajiwa kufungwa kuanzia Januari mwaka 2027.
Aidha, sheria hiyo itakwenda sambamba na marufuku ya matumizi ya simu za mkononi katika shule za sekondari.Hatua hiyo imekuja kufuatia ongezeko la wasiwasi kuhusu athari za mitandao ya kijamii kwa afya ya akili na maendeleo ya watoto.
Mamlaka ya afya ya umma nchini Ufaransa imewahi kuonya kuwa majukwaa kama TikTok, Snapchat na Instagram yanaweza kuwa na madhara kwa vijana, hususani wasichana, ingawa si sababu pekee inayochangia changamoto za afya ya akili zinazowakabili.
Sheria hiyo pia imeweka msamaha kwa baadhi ya majukwaa ya kielimu na tovuti za maarifa kama ensaiklopidia za mtandaoni.Ufaransa itaungana na zaidi ya nchi 20 duniani ambazo zimeanza kuweka masharti ya kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto.
Mwaka jana (2025) Australia iliongoza kwa kuwa nchi ya kwanza duniani kuzitaka kampuni za mitandao ya kijamii kufuta akaunti za Watoto walio chini ya miaka 16 au kukabiliwa na adhabu kubwa za kifedha.