MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ameipinga vikali Jumuiya ya Madola kwa kile alichokiita kujaribu kuiamrisha Tanzania katika masuala yake ya ndani, akisisitiza kuwa nchi hii ni taifa huru linalojitawala. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza katika mahojiano maalum na kituo cha runinga cha ITV siku ya Jumatatu, Wasira ameeleza kuwa Tanzania si kisiwa na iko tayari kuzungumza na kusikiliza ushauri kutoka kwa washirika wa kimataifa kama Umoja wa Ulaya, Marekani, Urusi na China, lakini haitakubali kupokea amri zinazovunja na kuingilia mamlaka yake ya ndani.
Mwanasiasa huyo mkongwe amesisitiza kuwa misingi ya kisheria na mhimili wa mahakama nchini lazima viheshimiwe bila kuingiliwa na shinikizo za nje:
“Hatujakataa kuridhiana, lakini Jumuiya ya Madola haiwezi kutuamrisha kuingilia Mahakama… kuna mambo wanaweza kutushauri na hatukatai kushauriwa, lakini haiwezi kutuamrisha, inakuwa inatuingilia uhuru wetu,” ameeleza Wasira.
Msimamo huo mzito wa Wasira unajiri siku chache baada ya Jumuiya ya Madola kutoa masharti ya siku 30 kwa Tanzania kushughulikia suala la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ambaye anashikiliwa gerezani akikabiliwa na mashtaka ya uhaini tangu mwezi Aprili mwaka 2025.