MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuchangia Baraza Kuu na chama, alipokuwa akiingia katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri la kikatiba Na. 7300/2026. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza kwa kifupi kabla ya kuingia mahakamani, Lissu alisema, “Changieni Baraza Kuu, changieni chama cha ukombozi.”Katika kikao cha leo, Lissu anatarajiwa kuendelea kuwauliza maswali ya dodoso mashahidi katika shauri hilo lililofunguliwa na mawakili Kulwa Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo.
Mawakili hao wanapinga hatua ya kuzuiwa kuingia Gereza la Ukonga na kukosa faragha ya kuzungumza na mteja wao, Tundu Lissu, waliporuhusiwa kumwona.
Jana, Lissu alikamilisha dodoso la shahidi wa kwanza ambaye ni Wakili Kulwa Maduhu, huku leo usikilizwaji wa shauri ukiendelea mbele ya jopo la majaji watatu linaloundwa na Jaji Amir Mruma, Jaji Dk. Angelo Rumisha na Jaji Dk. Evaristo Longopa.
Katika maendeleo mengine, Mahakama imemruhusu Lissu kukaa kwenye meza na kiti maalumu badala ya kizimba, kufuatia maelekezo yaliyotolewa jana kwamba shauri linaloendelea ni la kikatiba na si la jinai, hivyo hakuna ulazima wa yeye kukaa kizimbani wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.