SHAURI la Kikatiba Na. 7300/2026 lililofunguliwa na Mawakili Kulwa William Maduhu, Nashon Nkung, na Paul Kisabo dhidi ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) na wenzake, limeendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Amir Mruma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
​Katika shauri hilo lililofunguliwa rasmi Masjala Kuu Dodoma, mawakili hao wa Tundu Lissu wanalalamikia kuzuiliwa pamoja na kunyimwa haki ya faragha wanapokwenda kumtembelea na kuzungumza na mteja wao katika Gereza la Kuu la Ukonga.
​Akihoji maswali ya dodoso kwa shahidi wa pili wa waleta maombi, Wakili Nashon Nkung, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu (ambaye ni mjibu maombi wa nne), ameunga mkono hoja za mawakili wake huku akiibua madai mazito dhidi ya Jeshi la Magereza.

Lissu ameeleza kuwa maafisa wa magereza wamekataa kumpatia nakala ya hotuba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Oktoba 29, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.
​Lissu amebainisha kuwa aliahidiwa na kuagiza mawakili wake wamletee nyaraka hiyo ili kumwezesha kujiandaa na utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili, baada ya Jamhuri kuwasilisha maombi ya kumuongeza shahidi anayelenga kumhusisha na vurugu za Uchaguzi Mkuu matukio yaliyotokea akiwa tayari yupo gerezani kwa miezi sita.
Hata hivyo, licha ya mawakili wake kuifikisha nyaraka hiyo gerezani, maafisa wa magereza wameizuia hadi leo.
​Katika hatua nyingine, Lissu amegusia namna viongozi waandamizi wa Chadema wakiwemo John Heche, John Mnyika, Amani Golugwa na mawakili wake akiwemo Dickson Matata, Deogratias Mahinyila na Gaston Garubindi walivyopigwa marufuku kumtembelea gerezani, jambo linalokwaza maandalizi ya utetezi wake kwani baadhi yao ni mashahidi wake kwenye kesi ya uhaini.
​Kwa upande wake, Wakili Nashon Nkung, aliyehojiwa kama shahidi leo Jumanne 21 Julai 2026, ameieleza Mahakama namna maafisa wa Magereza Ukonga wanavyompekua, kumpa onyo, na kumnyima faragha ya kuzungumza na mteja wake kitendo alichokosoa kuwa ni kinyume cha miongozo, sheria, na kanuni zinazosimamia mawakili na magereza.