MWENYEKITI wa State Oil (T) Ltd, Nilesh Suchak kupitia kampuni ya uwakili ya Prime Attorneys, amemtumia barua Habibu Mchange wa Jamvi la Habari akimtaka kuomba radhi na kufuta kauli zinazodaiwa kuwa za kashfa zilizochapishwa na kurushwa kupitia vyombo vya habari mtandaoni.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Barua hiyo yenye tarehe 14 Julai 2026 inaeleza kuwa machapisho hayo yalichafua jina na hadhi ya mteja wao kwa kumhusisha na vitendo vya udanganyifu bila msingi.
Kwa mujibu wa barua hiyo, wakili anadai kuwa taarifa zilizochapishwa tarehe 11 na 13 Julai 2026 pamoja na makala nyingine zilizofuata zilitoa taswira inayomwonyesha Nilesh Suchak na kampuni yake kuwa wanajihusisha na vitendo vya kifisadi na udanganyifu.
Pia imeelezwa kuwa madai hayo yalichapishwa kwa nia ya kuharibu sifa na heshima ya mteja wao mbele ya umma.
Kutokana na madai hayo, Prime Attorneys wamemtaka mpokeaji wa barua hiyo kusitisha mara moja uchapishaji wa taarifa zinazodaiwa kuwa za kashfa, kuchapisha radhi na marekebisho ya taarifa hizo kwa namna ileile zilivyochapishwa awali, pamoja na kulipa fidia ya Shilingi bilioni 12 kwa madai ya uharibifu wa sifa na hadhi ya mteja wao.
Aidha, barua hiyo imeonya kuwa endapo matakwa hayo hayatatekelezwa ndani ya siku 14 tangu kupokelewa kwa barua, mteja wao ataanzisha hatua za kisheria bila kutoa taarifa nyingine, akidai fidia pamoja na gharama nyingine zitakazotokana na shauri hilo.
Hata hivyo, barua hiyo inaonyesha upande wa wadai pekee.
Kufuatana na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari, msimamo au majibu ya Habibu Mchange na Jamvi la Habari kuhusu tuhuma hizo bado hayajawekwa wazi, hivyo yatakapopatikana yatachangia kuleta uwiano wa taarifa kwa umma.