Rais Samia Suluhu Hassan
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa kupinga uteuzi wa Makamishna wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, maarufu kama Tume ya Jaji Lila.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Wilbert Chuma aliyekuwa akisikiliza shauri hilo lililofunguliwa na Bubelwa Ephraim Bubelwa pamoja na Joseph Daudi Mabugo, waliokuwa wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu.
Walalamikaji hao walitaka mahakama itengue uamuzi wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wa kuunda tume hiyo.
Walidai kuwa Rais hakuwa na mamlaka ya kuunda tume nyingine baada ya kukamilika kwa kazi ya Tume ya Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, iliyochunguza matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29, 2025.
Kesi hiyo ilifunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Tume Jaji Shaban Ally Lila, na Makamishna ambao ni Majaji Wastaafu, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Hata hivyo, Jaji Chuma ameweka wazi kuwa Rais anayo mamlaka kamili ya kisheria kuunda tume hiyo chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi.
Alifafanua kuwa ili tume ianze kazi rasmi ni lazima itangazwe kwenye Gazeti la Serikali na wajumbe wake waape viapo vyao, hatua ambazo bado hazijafanyika, na hivyo kufanya kesi hiyo kuletwa mahakamani kabla ya wakati.
“Hivyo malalamiko haya juu ya uhalali wa tume hii yameletwa kabla ya wakati, Mahakama hii inaona kwamba maombi haya yamekosa mashiko na inayatupilia mbali.”
Tume hiyo iliundwa na Rais Samia kufuatia mapendekezo ya ripoti ya Jaji Chande iliyowasilishwa 23 Aprili 2026, huku uteuzi wa viongozi wa tume hii mpya ukitangazwa rasmi 18 Mei 2026.