KIONGOZI Mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameibua mjadala kuhusu utekelezaji wa sheria nchini, akitaka maelezo ya kwanini vyombo vya dola havijamkamata mtu anayejulikana kama Mwaipopo anayetuhumiwa kuunda kikundi cha kijeshi kinyume cha katiba.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
​Zitto ametoa kauli hiyo 13 Julai 2026, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, ambapo alionyesha kushangazwa na ukimya wa mamlaka dhidi ya tuhuma hizo nzito wakati viongozi wa upinzani wakikabiliwa na ukamataji wa haraka.
Mwanasiasa huyo amemtolea wito wa dharura Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ili kunusuru mwelekeo wa haki na demokrasia nchini.
​”Yule Mwaipopo aliyeunda kundi la kijeshi kinyume cha katiba na sheria hatujaona hatua yeyote dhidi yake! Yupo juu ya sheria? Kwanini hajakamatwa?” amehoji Zitto, akitaka usawa katika kusimamia sheria za nchi bila kujali itikadi au upande anaotoka mtuhumiwa.
​Kiongozi huyo amesisitiza kuwa ili kuirudisha nchi katika mstari wa utulivu na maridhiano ya kisiasa yaliyokuwepo kati ya mwaka 2021 na 2023, hatua ya kwanza na ya haraka inayopaswa kuchukuliwa na serikali ni kumuachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Tundu Lissu.
Amesema hatua hiyo ndiyo itakayokuwa mwanzo wa kuiponya nchi dhidi ya migawanyiko inayozidi kujitokeza hivi sasa.