RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amesema kuwa mjadala unaoendelea kuhusu makala za Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) haupaswi kuwa kipaumbele cha serikali, kwani maudhui yaliyoandikwa na chombo hicho ni kidogo sana ikilinganishwa na ukubwa wa changamoto halisi za kiutekaji na uvunjifu wa sheria zilizopo nchini.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
​Kupitia taarifa aliyoitoa leo 14 Julai 2026, Wakili Mwabukusi ameeleza kuwa badala ya mamlaka kukimbizana na kupingana na makala za nje, zinapaswa kujikita katika kutatua vyanzo vya hasira na maumivu ya wananchi vinavyotokana na mifumo ya ndani kushindwa kusimamia haki na utawala wa sheria.
​”Haya mambo yote yanakiuka hata Katiba hii tuliyonayo wala hatuhitaji kukimbizana na Makala za BBC kwani zimeandika kidogo sana kuliko uhalisia,” amesisitiza Mwabukusi katika taarifa yake, huku akiongeza kuwa hata kauli za vyombo vya kimataifa kama Jumuia ya Madola (Commonwealth) ni ukumbusho tu wa misingi ya haki za binadamu iliyoainishwa tayari kwenye Ibara ya 13 hadi 29 za Katiba ya Tanzania.
​Mwabukusi amebainisha kuwa nchi haiwezi kukwepa ukweli huo kwa kubishana na vyombo vya habari vya kigeni wakati kuna matukio ya wazi ya utekaji, upotezwaji wa watu kama akina Soka, Mdude na Chaula, pamoja na ubaguzi katika ukamataji wa viongozi wa kisiasa kama Tundu Lissu huku watuhumiwa wengine wakiachwa huru.
Ameitaka serikali kuelekea kwenye misingi ya ukweli na uwajibikaji kwa kuunda Tume ya Ukweli (Truth Commission) ili kutatua migogoro hiyo badala ya kufanya propaganda dhidi ya ripoti za nje.