WAZIRI wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan, kutumia hekima na busara alizoonyesha wakati wa kutangaza sera ya 4Rs kwa kumwachia huru Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wake wa X leo 13 Julai 2026, Prof. Tibaijuka amesema anaendelea kusisitiza kuwa Lissu aachiwe huru kwa kuwa, kwa mtazamo wake, kesi inayomkabili haikamiliki.
“Rais Samia naendelea kushauri kwa dhati Tundu Lissu aachiwe huru kwani kesi haikamiliki,hekima na busara iliyokufanya kutangaza sera ya 4Rs mara ulipoingia madarakani ikuongoze tena katika jambo hili,” ameandika Tibaijuka
Aidha, Prof. Tibaijuka amesema simulizi zinazoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu suala hilo zinaibua hisia kali kwa wananchi, hususan vijana, na kwamba hata wazee wamekumbushwa matukio ya Operesheni Sogeza iliyohusisha uundaji wa Vijiji vya Ujamaa kati ya mwaka 1974 na 1976.
Ameeleza kuwa taarifa hizo zina athari kwa taswira ya Tanzania na maslahi ya taifa, akisisitiza kuwa ni muhimu kutafuta muafaka kupitia uwajibikaji na maridhiano.
Prof. Tibaijuka pia ametoa wito kwa viongozi na wananchi kuwa na hofu ya Mungu, kutambua miujiza yake na kuliombea taifa kwa imani za kila mmoja.
“Tuwe na hofu ya Mungu na kutambua miujiza yake, mfano wa risasi 16 kushindwa kukomesha uhai ingawa maumivu ni makubwa. Tutubu na kusali kuliombea Taifa letu kila mtu kwa imani yake,” amesema.