ALICIA Lissu, mke wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amesema familia yake inapitia kipindi kigumu cha kiuchumi na kisaikolojia tangu mumewe alipokamatwa na kuwekwa kizuizini mwezi Aprili 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza katika mahojiano na BBC Africa Eye, Alicia alisema amejikuta akibeba jukumu lote la kulea watoto na kugharamia mahitaji ya familia bila msaada wa mumewe, hali ambayo amesema haikuwa rahisi kuizoea.
“Kwa mara ya kwanza kabisa, nilijikuta kuwa sina msaada wowote kutoka kwa Lissu. Hakuwepo na pia hakuna msaada wa kifedha. Ninalazimika kujitunza pamoja na kuwalea watoto wetu,” alisema Alicia.
Alieleza kuwa kutokana na mazingira ya kizuizini, hajapata nafasi ya kuzungumza wala kukutana na mumewe kwa muda mrefu, jambo ambalo amesema limeongeza mzigo wa kihisia kwa familia yao.
Kwa mujibu wa Alicia, watoto wao wanaosoma nchini Marekani wameendelea kuishi katika hofu na wasiwasi kuhusu hali ya baba yao, huku yeye akijitahidi kuwapa utulivu na kuendelea kusimamia maisha ya familia.
Licha ya changamoto hizo, Alicia alisema bado anaendelea kujivunia msimamo wa mumewe, akimtaja kuwa kiongozi jasiri ambaye hajawahi kuyumba katika kutetea anachoamini.
Alikumbusha pia kuwa familia yao imepitia nyakati ngumu hapo awali, ikiwemo shambulio la risasi dhidi ya Tundu Lissu mwaka 2017.
Tundu Lissu alikamatwa wakati wa kampeni ya “Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi” na kwa sasa anakabiliwa na shtaka la uhaini. Chini ya sheria za Tanzania, kosa hilo halina dhamana na shauri lake linaendelea kusikilizwa mahakamani.
Kwa upande wake, Serikali ya Tanzania imesema hatua zinazochukuliwa dhidi ya Lissu zinafuata sheria za nchi na kwamba kesi hiyo ipo mikononi mwa mahakama, hivyo haiwezi kuingiliwa kisiasa.