MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameiomba Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kuiomba mahakama iamuru alipwe fidia kutokana na kile alichodai kuwa ni ucheleweshaji wa makusudi wa shauri lake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Lissu alitoa maombi hayo mbele ya jopo la Majaji wa Rufani Shimwa Mwarija, Muruke na Khamis, akidai kuwa maombi ya DPP yamekuwa yakitumika kurefusha kesi ya msingi na kumfanya aendelee kukaa gerezani bila sababu za msingi.
Alidai kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa kesi yake kwa siku 139 tangu 24 Februari 2026 hadi 3 Julai 2026, huku akisema amekuwa mahabusu kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu.
Kwa mujibu wa Lissu, hatua hiyo ya DPP inakwenda kinyume na wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha mwenendo wa mahakama hautumiki vibaya na kwamba maslahi ya umma yanazingatiwa katika uendeshaji wa mashauri.
Lissu alihoji ni maslahi gani ya umma yanayopatikana kupitia maombi hayo na kuiomba Mahakama ya Rufani kuyatupilia mbali pamoja na kumuamuru DPP kumlipa fidia kwa usumbufu alioupata kutokana na ucheleweshaji huo.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, alipinga madai ya Lissu akisema kuwa maombi yaliyowasilishwa na DPP hayakulenga kuchelewesha kesi hiyo.
Katuga pia alipinga ombi la fidia, akieleza kuwa kifungu cha sheria alichokitaja Lissu hakitumiki katika mazingira ya shauri hilo, akifafanua kuwa masharti hayo hutumika pale ambapo mahakama inakuwa imesikiliza shauri na kubaini kuwa halina msingi.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote kuhusu pingamizi la awali na maombi ya msingi, Mahakama ya Rufani iliahirisha shauri hilo na kueleza kuwa itatangaza tarehe ya kutoa uamuzi wake baadaye.