Salum Mwalimu, Katibu Mkuu wa Chaumma
KATIBU Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amegoma kung’olewa kwenye wadhifa wake, badala yake amemtaka mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe, kuunda tume ya uchunguzi dhidi yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Katiba barua yake kwa Rungwe, aliyomtumia leo Jumanne, tarehe 30 Juni, Mwalim anasema, “Nakuandikia kama rejea rasmi ya ombi langu mbele ya Kamati Kuu jana (tarehe 29 Juni 2026), kuhusu Kamati Kuu kuunda timu ya kuchunguza yaliyosemwa na baadhi ya wajumbe juu yangu.
“Kwamba kama nilivyotamka jana, nitakuwa tayari kujibu yale yatakayothibitika na hata kuwajibika nayo,” ameeleza mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mgombea urais wa chama hicho, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.
Hatua ya Mwalim kumuandikia barua mwenyekiti wake, imekuja siku moja baada ya baadhi ya wajumbe wa sekretarieti, waliongozwa na Benson Kigaila, naibu katibu mkuu Bara, kumtuhumu kuendesha chama kama mali yake binafsi.
Kigaila na wenzake, walijiorodhesha mbele ya Kamati Kuu, wakidai kuwa hana tena imani na katibu mkuu wao na kwamba wanaiomba Kamati Kuu, kumhoji na kumuondoa kwenye wadhifa wake.
Akiandikwa kwa unyenyekevu mkubwa kwa mwenyekiti wake, Mwalim anasema, “kama nilivyoomba kwako na mbele ya Kamati Kuu yako jana, nitakaa nje ya ofisi kutoa nafasi na uhuru wa uchunguzi huo, hadi hapo suala hili litakapomalizika.”
Anasema, “Na iwapo utaridhia, nakaimisha nafasi yangu ya Katibu Mkuu kwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila.”
Akaongeza, “Nakutakia majukumu mema. Wasalaam, Salum Mwalim, Katibu Mkuu Juni 30, 2026.”
Miongoni mwa yaliyojiri kwenye kikao hicho na ukweli wa sakata lenyewe jinsi lilivyosukwa, lilivyoratibiwa na jinsi lilivyotelelezwa, soma gazeti la MwanaHALISI, Alhamisi hii – Mhariri.