JESHI la Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU), kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu waliokuwa wakijaribu kutorosha mifugo, Ngo’mbe, Mbuzi na Kondoo 852 kwenda nchi jirani kinyume cha sheria.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kamanda wa Kikosi hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Simon Pasua, mapema leo amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumefanyika wakati wa doria ya pamoja katika Kijiji cha Matelea, Kata ya Matelea, Wilaya ya Longido Mkoani Arusha.
Kamanda Pasua amesema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa taratibu nyingine za kisheria, huku akitoa wito kwa Wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kufuata sheria pindi wanaposafirisha mifugo kwenda nchi jirani ili kuepuka usumbufu unaoweza jitokeza.
Aidha Kamanda huyo ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu hususani wanaposafirisha mifugo kinyume cha sheria, kwani pamoja na kwamba wanalikosesha taifa mapato lakini pia ni chanzo cha kuenea kwa magonjwa ya mifugo na ukiukwaji wa haki za wanyama.