MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, leo 8 Juni 2026, inasikiliza shauri la maombi ya ruhusa ya kupinga Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Tume hiyo, inayojulikana kama Tume ya Jaji Lila, iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, huku mwenyekiti na wajumbe wake wakitangazwa rasmi 18 Mei 2026.
Tume hiyo inaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Lila, akisaidiwa na majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao ni Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Rais Samia aliunda tume hiyo kufuatia mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman.
Hata hivyo, kabla ya tume hiyo kuanza rasmi kazi zake, mwanaharakati Buberwa Buberwa na mwenzake Joseph Mabugo wamefungua shauri mahakamani wakipinga uhalali wake.
Waombaji hao wanawakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu.
Shauri hilo linasikilizwa na Jaji Augustine Rwizile ambaye katika hatua ya awali ataamua iwapo waombaji wanastahili kupewa ruhusa ya kufungua shauri rasmi la kuipinga tume hiyo au la.