KAMPUNI ya Barrick nchini Tanzania, imedhamini na kushiriki katika kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati vilivyopo mkoani Mwanza lililoandaliwa na taasisi ya kuchipua na kuendeleza vipaji vya uongozi kwa vijana (AIESEC Tanzania) lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine jijini Mwanza na kuwashirikisha wanafunzi,wahadhiri na wadau mbalimbali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Taasisi ya AIESEC inasifika kwa mchango wake mkubwa wa kuwajengea uwezo vijana ili kuwa viongozi bora na mahiri duniani kwa miaka ijayo. Nchini Tanzania pia taasisi hiyo inafanya kazi kwa kuwakutanisha vijana wenye ndoto kubwa ya kupata mafanikio katika maisha baada ya kumaliza masomo yao.
Kupitia kongamano hili ambalo hufanyika kila mwaka, wanafunzi huweza kufahamu jinsi taasisi mbalimbali nchini zinavyoendesha shughuli zake lengo kubwa ikiwa ni kuwajengea uwezo wa kujua vipaji walivyonavyo, kujifunza jinsi ya kujiamini na kukabiliana na ushindani katika soko la ajira, kujitambua uwezo wao ni jinsi gani wanaweza kushiriki kutoa mchango wa kuendeleza taifa pindi wamalizapo masomo yao.

Wataalamu mbalimbali walitoa mada za kuwajengea uwezo Wanafunzi kusoma kwa bidii na kuzidi kuwa wabunifu ili waweze kwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia na kidigitali ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za ajira zinazojitokeza na pia kuwa na uwezo wa kujiajiri na kuzalisha ajira.
Maofisa Waandamizi wa Barrick pia walishiriki katika maonesho na kongamano hilo ambapo walipata fursa kuzungumza na wanafunzi kuhusiana na kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ajira,kuendeleza vipaji vyao pia wanafunzi walipata fursa kuelewa jinsi kampuni ya kimataifa ya Barrick, inavyoendesha shuguli zake kwa kutoa kipaumbele kusaidia jamii sambamba na mpango wake wa kuibua na ukuzaji wa vipaji kwa vijana wa kitanzania na wafanyakazi wake na mpango wa kampuni wa kufanikisha kutekeleza malengo endelevu ya milenia.