BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua kampeni ya “Tunakuona Mbali” yenye lengo la kuwawezesha Watanzania kufikia malengo yao ya maendeleo kupitia huduma rasmi za kifedha, huku ikichochea ujumuishaji wa kifedha na ukuaji wa uchumi jumuishi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa NBC, David Raymond, alisema kampeni hiyo inalenga kuwasaidia wananchi kujenga utamaduni wa kuweka akiba, kuwekeza, kupata mikopo na kutumia huduma za kifedha kwa ufanisi ili kutimiza ndoto zao za maisha na biashara.
Alisema NBC inatoa suluhisho mbalimbali vya kifedha kwa makundi tofauti ya jamii ikiwemo watoto, vijana, wanawake, wafanyakazi, wanafunzi, vikundi, wafanyabiashara na Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Kampeni hiyo pia itatoa elimu ya kifedha kuhusu usimamizi wa fedha, matumizi sahihi ya mikopo, bima, uwekezaji na huduma za kidigitali.
Kwa upande wake, Meneja wa Bidhaa na Mauzo wa NBC, Dorothea Mabonye, alisema huduma za benki hiyo zimebuniwa kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali na kuwawezesha wananchi kupanga na kufanikisha malengo yao ya kifedha.
Naye Mkuu wa Huduma za Kidigitali wa NBC, Ulrik Peter, alisema benki hiyo imeendelea kuwekeza katika teknolojia kupitia huduma kama NBC Kiganjani, NBC Connect, kadi za benki na mtandao wa mawakala ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha popote na wakati wowote.
Kupitia kampeni ya “Tunakuona Mbali”, NBC inalenga kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuwajengea wananchi uwezo wa kufanya maamuzi bora ya kifedha na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa