Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TACAS) kimesema pendekezo la ada ya asilimia 4.5 ya uendelezaji wa Miundombinu mipya ya Bandari (PID) inalenga kusaidia maboresho makubwa ya bandari nchini ili kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji wa mizigo. Anaripoti Mwandishi Wetu…..(endelea)
Hayo yameelezwa mkoani Mtwara hivi karibuni wakati wa Mkutano wa Wadau wa Watumiaji wa Bandari ya Mtwara, ambapo Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TACAS) na wafanyabiashara wameunga mkono tozo hiyo kufuatia punguzo hilo la kipekee lililolenga kulinda mitaji na kuzuia mfumuko wa bei wa bidhaa mtaani.
Mwenyekiti wa TACAS, Ephraim Mwankusye, amebainisha kuwa tofauti na tozo zingine, makusanyo ya PID yanasimamiwa kisheria kwenda moja kwa moja kwenye ujenzi wa miundombinu mipya na hakuna fedha itakayopotea kwenye matumizi ya kawaida ya kiutawala.
Amesema fedha hizo zitaelekezwa kwenye upanuzi wa magati na reli kwenye bandari za kimkakati za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, maendeleo ya Bandari ya Bagamoyo, ujenzi wa matenki ya kisasa ya kuhifadhia mafuta (Oil Terminals) na barabara unganishi za kupitishia mizigo minene ili kuongeza kasi ya upakuaji.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, amefafanua kuwa awali serikali ilitaka kuanza kukusanya tozo hiyo ya asilimia 9 mwezi Machi 2026, lakini ikalazimika kupiga breki ili kutoa nafasi ya kusikiliza maoni ya wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara nchini kabla ya kufikia makubaliano ya kuanza kutumika Julai mwaka huu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Mtwara, wadau wa usafirishaji wamesema kuwa maboresho hayo yataleta mapinduzi makubwa kwani yataongeza kasi ya kutoa mizigo bandarini, kupunguza gharama za meli kusubiri nangani (Demurrage charges), na kuongeza ushindani wa Tanzania dhidi ya bandari zingine za ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (EAC & SADC).
Baada ya kusitishwa kwa miezi mitatu kupisha majadiliano, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilitangaza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Ada ya Uendelezaji wa Miundombinu Mipya ya Bandari (Port Infrastructure Development Fee – PID) kuanzia Julai 1, 2026, huku kiwango chake kikishushwa kwa nusu kutoka asilimia 9 hadi asilimia 4.5 ya kodi ya forodha.