ALIYEKUWA Mbunge wa Iringa Mjini kupitia CHADEMA, Peter Msigwa, amesema vyombo vya dola, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za uchaguzi vinapaswa kutenda kazi kwa usawa kwa maslahi ya wananchi wote badala ya kupendelea upande mmoja wa kisiasa.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Msigwa amesema changamoto kubwa iliyopo ni pale taasisi muhimu za nchi zinaposhindwa kusimamia haki na usawa, akisisitiza kuwa mahakama imara ni msingi wa utawala bora na maendeleo ya taifa. Alieleza kuwa nchi haiwezi kusimama imara ikiwa mfumo wa utoaji haki ni dhaifu.
Akizungumza baada ya kurejea Chadema, Msigwa amesema anafurahia kurudi “nyumbani” na kwamba hajarejea kwa lengo la kutafuta cheo chochote bali kushiriki katika kujenga chama na kuwatumikia wananchi.
“Nimefurahi sana kurudi nyumbani. Sijaja kutafuta cheo chochote, nimekuja kufanya kazi na kujenga chama. Pamoja na kosa nililolifanya kwenda CCM, nimejifunza mengi na ninaweza kutumika zaidi,” amesema Msigwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kujenga siasa za hoja nchini, akieleza kuwa wananchi wanahitaji mijadala yenye kuzingatia masuala ya maendeleo, uwajibikaji na ustawi wa taifa badala ya siasa za migogoro na malumbano yasiyo na tija.