SERIKALI imetangaza kuundwa kwa Tume maalum ya Uchunguzi itakayochunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Hatua hiyo imekuja kufuatia mapendekezo ya Tume ya Rais iliyoshauri kufanyika kwa uchunguzi maalum kuhusu vurugu zilizoripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini kipindi cha uchaguzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo 18 Mei 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses M. Kusiluka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametumia mamlaka yake chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, kuunda tume hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Shabani Ally Lila ameteuliwa kuwa Kamishna na Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Wajumbe wengine walioteuliwa ni Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir pamoja na Aishieli Nelson Sumari.
Tume hiyo itakuwa na jukumu la kuchunguza chanzo cha ghasia hizo, madhara yake pamoja na kutoa mapendekezo ya hatua za kisheria, kiutawala na kiusalama ili kuzuia matukio kama hayo katika chaguzi zijazo.
Serikali imesema hatua hiyo inalenga kuimarisha demokrasia, kulinda utawala wa sheria na kuhakikisha uchaguzi nchini unafanyika kwa uhuru, haki na amani.