MWENYEKITI wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema kuna umuhimu wa kufanyika mjadala wa Kitaifa kuhusu mustakabali wa Nchi kufuatia Ripoti ya Jaji Othman Chande iliyohusu vuguvugu la Oktoba 29, 2025.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza leo 16 Mei 2026 Jijini Dar es Salaam wakati wa Mjadala wa Kitaifa kuhusu Mwelekeo na Hatma ya Tanzania, Othman amesema chama chake kimeamua kuandaa mjadala huo ili kutoa nafasi kwa Watanzania na wadau mbalimbali kutafakari kuhusu hali ya Taifa na mwelekeo wake wa baadaye.
“Ni mara ya kwanza kwa chama chetu kuandaa mjadala wa Kitaifa wa namna hii, tumefanya hivi kama tulivyoelekezwa kufanya tafakuri kuhusu Nchi yetu tulipotoka, ilipo sasa na yale tunayoyaona kuhusu mustakabali wa Taifa letu,” amesema Othman.
Amesema bado kuna sintofahamu kuhusu mwelekeo wa Taifa baada ya matukio yaliyopita pamoja na Ripoti ya Jaji Chande, hali ambayo imeongeza umuhimu wa kuwa na mjadala mpana wa Kitaifa.
“Niseme kwa ufupi, bado tunaona kiza kinene kimetanda, na bado kipo mbele yetu, kwasababu hiyo tukaona sisi kama sehemu ya kutekeleza wajibu wetu wa Kikatiba kama Chama cha Siasa na kama sehemu ya Watanzania, tuchukue hatua hii ya kuwaomba wenzetu pamoja na wadau mbalimbali tushirikiane kuutazama mustakabali wa Nchi yetu,” amesema Othman.
Othman ameongeza kuwa mjadala huo unalenga kusaidia Taifa kupata mwelekeo mwema baada ya changamoto zilizopita na kuibua mjadala mpana kuhusu hatma ya Tanzania.