Zitto Zuberi Kabwe
ZITTO Zuberi Kabwe, mwanasiasa mashuhuri nchini na mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), amemuonya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwamba aache kukisakama Chadema. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akiandika kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X, leo Alhamisi 14 Mei 2026, Zitto amemtaka Jaji Mutungi kuacha kukisakama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Amesema, “kitishi chochote dhidi ya Chadema, ni tishio la demokrasia nchini” na kuongeza,
“Zile zama za ofisi ya msajili wa vyama kuwa mchezaji namba 12 wa CCM FC, sasa zimekwisha.”
Amesema, “Dola (serikali) isome alama za nyakati. Msajili kutaka kufuta Chadema, kutakufanya ufutwe wewe. Tume ya Jaji Othman Chande, iliyoundwa na Rais imetoa taarifa inayosema wananchi wanailalamikia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutokutenda haki kwenye kusimamia shughuli za vyama. Tafadhari usirudie makosa ya nyuma.
Zitto anasema, Msajili anapaswa kuchutama, kuwajibika na kubadilika, badala ya kurudia baadhi ya makosa ya ubaguzi na kutotenda haki kwa vyama vya siasa nchini kama ilivyoelezwa katika ripoti ya Tume ya kuchunguza ghasia za wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba.
“Msajili anajua, Watanzania wanajua na dunia inajua, kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kufanya makosa makubwa kuliko hata ambayo ameituhumu Chadema. Lakini hawajawahi kuona hatua zikichukuliwa dhidi ya chama hicho,” amefafanua.
Anasema, ofisi ya Msajili inafahamu kwamba wananchi sio mabwege, na kwamba wanalichukulia tishio lolote dhidi ya Chadema kuwa kitisho dhidi ya demokrasia na utawala bora.
Anasema, “…iacheni CCM ifanye siasa za ushindani dhidi yetu. Nasi tufanye siasa za ushindani dhidi yao. Acheni kuwa mbeleko yake. Mtaanguka nayo. Ujumbe huu sio wa Msajili tu bali pia ni kwa vyombo vya ulinzi na usalama pia. Kaeni pembeni, acheni vyama vya siasa vifanye siasa.”
“Mpango wako wa kutaka kuifuta Chadema, utafutwa wewe na hakuna shaka kuhusu hili,” amesisitiza.
Kauli ya Zitto imekuja siku moja, baada ya Chadema kuripoti kuwa Msajili amewalima barua ya kutaka wajieleze kwanini wasisimamishwe kufanya shughuli za kisiasa au kutozwa faini, kufuatia tuhuma kuwa wamekiuka sheria ya vyama vya siasa na kuhatarisha amani, usalama na utulivu wa nchi.
Msajili ameeleza katika barua yake kwa Chadema, kwamba amekuwa akifuatilia kwa karibu mwenendo wa viongozi wake, kauli zao katika mikutano ya hadhara, taarifa za vikao vyao pamoja na maudhui yanayosambazwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa hoja zilizotajwa kwa uzito mkubwa ni kauli zinazodaiwa kutolewa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara, John Heche, kwamba wataitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kuachiwa huru kwa Tundu Lissu, mwenyekiti wa chama hicho, taifa.