CHAMA cha ACT Wazalendo kimeshikilia msimamo wa kutofautiana na mtizamo wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 nchini Tanzania, na kimetanua wigo kwa kumtetea Jaji mstaafu Joseph Warioba anayelalamika kutishiwa maisha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Wenyeviti wa mikoa 11 ya kichama wa ACT Wazalendo upande wa Zanzibar wamesema wanaunga mkono maazimio yaliyotolewa na Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu ripoti aliyowasilisha Jaji Mohamed Othman Chande, Mwenyekiti wa Tume ya Rais iliyochunguza matukio hayo, wakisema wanaridhika kuwa tume hiyo imesaliti Watanzania.
Kitendo cha Tume hiyo kukwepa kuwajibisha waliohusika na vurugu na mauaji ya raia ni usaliti dhidi ya wananchi na wenyeviti hao wanatoa rai kuwa lazima uchunguzi mpya ufanywe na tume iliyo huru pamoja na kuachiwa kwa watu waliofunguliwa kesi za kisiasa wakihusishwa na matukio hayo.
“Tunakipongeza Chama chetu kwa kusimama upande wa haki na kutowasaliti Watanzania… tunasisitiza wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wale wote waliotajwa kwenye Azimio la Kamati Kuu wanapaswa kuwajibika.
“Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa {DGTIS}, Mkuu wa Jeshi la Polisi {IGP}, Msajili wa Vyama vya Siasa, Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, wakuu wa mikoa iliyohusika na mauaji ya wananchi wawajibishwe.”
Tamko la wenyeviti hao lililosomwa mbele wakati wa mkutano na waandishi wa habari Ofisi Ndogo ya chama Vuga, mjini Zanzibar, limeitaja mikoa husika na viongozi wake kuwa ni Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Mwanza, Geita, Arusha, Iringa, Dodoma, Shinyanga, Mara na Ruvuma.
Pia tamko likataja pia wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na wilaya za Mbeya, Mbeya Vijijini, Kyela, Mbozi, Momba, Nyamagana, Ilemela, Geita, Arumeru, Arusha, Iringa, Dodoma mjini, Kahama, Musoma, Tarime, Bunda na Songea ambako matukio ya mauaji raia yalishamiri kuwa nao wawajibishwe.
“Tunaunga mkono azimio la KK ya Chama la kuhitaji kuanza mchakato wa Katiba mpya, mageuzi ya Jeshi la Polisi na kufutwa sheria zote kandamizi ikiwemo Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa, na sheria 40 zilizotangazwa na Tume ya Jaji Nyalali ya mwaka 1992, kuwa ni sheria kandamizi.
Mbali na nasaha za kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuiweka hadharani ripoti ya Tume ya Jaji Chande, wenyeviti wa mikoa wa ACT Wazalendo wanatangaza kulaani wote wanaomtishia Waziri Mkuu mstaafu na Jaji Warioba ambaye ametoa maoni ya kulalamikia ripoti ya tume ya Jaji Chande. “Tunakemea kwa nguvu zote vyombo vya dola kumtisha au kumshurutisha Jaji Warioba {ili} asisimame kwenye ukweli.
“Tunapenda kutuma ujumbe kwao kuwa ukweli haufichiki kamwe, unaweza kuuficha kwa muda lakini si milele. Tunatuma salam za mshikamano na kumpa moyo Waziri Mkuu mstaafu Warioba kwa kuwa sehemu ya viongozi wastaafu waandamizi waliosimamia ukweli kwenye suala la ripoti ya Jaji Chande,” tamko limesema na kuzipongeza asasi na mashirika ya hiyari yaliyosimama kwenye ukweli kuhusu suala hilo.
Wametaja Kituo cha Huduma za Sheria na Haki za Binaadam {LHRC}, Chama cha Wanasheria Tanganyika {TLS}, Centre for Strategic Litigation {CSL}, Twaweza EA, Affirmative Action on Gender Equality Network {AGEN}, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadam {THRDC}, Tanzania Transparency Forum {TRFO}, Juwkaa la Katiba Tanzania, ForDia, NACOCET, Muungano wa Vyama vya Wavuvi Tanzania {FUO}, PINGOs Forum, Center Against Gender Based Violence {CA-GBV} na Tanzania Child Welfare {TCW}.