Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini kwa kuongeza usahihi wa utabiri, kufunga mitambo ya kisasa na kuendeleza mifumo ya tahadhari za mapema dhidi ya majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa. Anaripoti Mwandisho Wetu, Dodoma … (endelea).
Hayo yameelezwa leo tarehe 13 Mei 2026, bungeni na Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo.
Profesa Mbarawa alisema TMA imeendelea kutoa huduma za hali ya hewa pamoja na kudhibiti na kuratibu shughuli zote zinazohusiana na hali ya hewa nchini, sambamba na kufanya tafiti za kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kubadilishana taarifa za hali ya hewa kimataifa kupitia mfumo wa Global Telecommunication System (GTS).
Alisema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika vifaa vya kisasa, mifumo ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa hali ya hewa, wastani wa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa umefikia asilimia 87.6 hadi Machi 2026, ikilinganishwa na asilimia 86 kwa kipindi kama hicho mwaka 2025.
“Ufanisi huu umesaidia kupunguza madhara yatokanayo na hali mbaya ya hewa ikiwemo vifo na upotevu wa mali,” alisema Profesa Mbarawa.
Katika kuendelea kuboresha huduma hizo, alisema TMA imekamilisha ufungaji wa mitambo nane ya kupima hali ya hewa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bukombe, Kahama, Hanang, Meatu, Unguja Kusini, Korogwe, Ikungi na Nanyumbu.