KILA nikitazama na kusikiliza minyukano ya maneno kati ya viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mbunge wa Rufiji na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa juu ya tuhuma za rushwa napata shida na malezi tuliyonayo kwenye jamii.Anaandika Salehe Mohamed … (Endelea)
Minyukano hiyo inatokana na kauli ya Mchengerwa aliyoitoa tarehe 6 Oktoba, 2026, alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Pwani katika Manispaa ya Kibaha, alisema;
“Nawashukuru UWT (Umoja wa Wanawake CCM) hamjachagua upande kama vijana (UVCCM), vijana wao wameamua kuchagua upande, Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) rushwa imezidi, jumuiya hii ina changamoto viongozi wote hawatufai. Tunajua siasa za rushwa ndizo zinakwenda kukiangusha chama hiki (CCM)”
“Sasa tunajua vijana wamekata tamaa kwa sababu viongozi wao wanashindwa kuwatetea kwasababu ya rushwa. Sasa hili lazima niliseme kwasababu mimi ninakemea rushwa. Kule Kisarawe Mwenyekiti na Katibu wa UVCCM wameitwa kwenye vikao vya maadili kwasababu ya rushwa.”
Mara baada ya kauli hiyo, si viongozi wala wanachama wa UVCCM waliokaa chini na kutafakari kwa kina juu ya rushwa. Kila waliyepata nafasi ya kusema au kuandika alimrushia mawe Mchengerwa kana kwamba alichokisema ni uongo.
Wanachokifanya viongozi wa UVCCM na wanachama wake kinanikumbusha kisa cha mbuni ayetumbukiza kichwa chake shimoni akiamini amejificha ilhali sehemu kubwa ya mwili wake iiwa nje.
UVCCM badala ya kufanyia kazi tuhuma zilizoelekezwa kwao wameamua kukataa na kumshambulia mtoa hoja na si hoja. Nani asiyejua rushwa ni donda ndugu kwenye nchi yetu na mifumo ya kisiasa?
Mchengerwa ni mzoefu ndani ya chama anajua sarakasi za kupata viongozi kuanzia ngazi za chini hadi juu, anajua vijana wanavyotumika kwa kuwa naye ni miongoni mwao. Anachokisema ana uhakika nacho, labda tatizo tu amekisema hadharani badala ya chumbani.
Nani asiyejua vijana wanavyopepea kwenye maeneo mbalimbali nyakati za uchaguzi kugawa na kupokea chochote. Kuna asiyejua hawa ndiyo injini ya kufanikisha ushindi wa kambi au chama fulani?
Kila mmoja wetu ni shahidi wa fedha zinavyomwaga nyakati za chaguzi iwe ndani ya chama au nje. Si mara kadhaa tumesoma na kusikia habari za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata wagombea na wapambe wao?
Nilifundishwa kuwa hoja inapaswa kujibiwa kwa hoja na si vioja, niliambiwa kamwe nisithubutu kumshambulia mtoa hoja balo hoja aliyoitoa kwa kuipatia majibu. Kila nikiona watu wanamshambulia mtoa hoja ninawaona hawajielekezi sawasawa.

Nawashangaa UVCCM wanaomvaa Mchengerwa wakati hata Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan alishakemea vikali vitendo vya rushwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa kupata wagombea wa chama hicho.
Aliweka bayana kwamba wagombea ubunge, udiwani, uwakilishi watapimwa kwa kazi walizozifanya wakati wapo madarakani, wala sio kwa khanga na elfu kumi, kumi wanazotoa kwa wajumbe wanaowapigia kura.
Hivi ni kijana gani mwenye ubavu anayeweza kusimama mbele ya hadhara akakataa nyakati za uchaguzi si mavuno kwao? Si ndiyo wanaotumika kusaka wajumbe na kuwalainisha kwa vipande vya fedha, khanga, kofia, fulana, mabati na ahadi kemkem.
Wakati wa uchaguzi ndiyo wakati wa toa ‘kula nikupe kura,’ huu ndiyo wakati wa mkono mtupwi haulambwi. UVCCM wanalijua hili vilivyo na hawana sababu ya kulikataa kama wanataka kujisafisha.
Kukivunja kioo kililichokuonesha u mchafu si njia ya kujisafisha bali ni kujidanganya na kuahirisha tatizo. Cha msingi ni kujisafisha sehemu zote chafu.
Inawezekana kabisa Mchengerwa, kaamua kupasua jipu hili hadharani baada ya kambi yake kupigwa dafrao katika kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho. Kama hivyo ndivyo, je hana hoja juu ya kukithiri kwa rushwa ndani ya UVCCM?
UVCCM ndiyo walinzi wa chama na wanakolelewa ili waje kuwa viongozi wa chama nan chi, kama watakulia katika misingi ya rushwa wakishapewa uongozi watawezaje kuondoka kwenye mfumo uliowakuza ambao ni adui wa haki?
Njia pekee ya kukabiliana na rushwa ni uwazi, kuwajibika na kuwajibishana. Yasipofanyika hayo kila kukicha tutaendelea kusikia vilivyo vya mara kwa mara vya kukosekana kwa haki kwenye jamii
Mwisho.
