WILLIAM Maduhu, Wakili Mwandamizi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), ameshangazwa kuona Mtanzania anayeunga mkono chama tawala akitishia kuondoa uhai wa Mtanzania mwingine mwenye mrengo bila kuchukuliwa hatua yoyote ya kisheria.Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Digital, Maduhu amesema kitendo cha mtu aliyejitambulika kwa jina la Hussein Kawambwa kutumia mtandao wa Facebook kumtishia maisha Deogratius Mahinyila, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), bila kuchukuliwa hatua yoyote.
“Huyu mtu kuonesha kuwa amekusudia na anachokifanya anakijua hajafuta ujumbe wake ule tangu alivyouchapisha jana mpaka hivi tunavyozungumza nilitegemea angeitwa polisi na kuhojiwa, angalau aulizwe alikuwa anakusudia nini lakini hakuna hatua yoyote ya kisheria imechukuliwa,”amesema Maduhu.
Ameeleza kuwa upande wa upinzani ukitoa kauli inayonekana kuwa na viashiria vya uchochezi hukamatwa na kufunguliwa kesi.
Maduhu amesema kuwa sheria ipo wazi kuwa yeyote atakemtishia mwenzake kumuua atahukumiwa mpaka miaka mitano jela.
“Wakati taarifa za matukio ya watu kutekwa na kupotea zikionekana kupungua kwa kiasi kikubwa inashangaza kuona bado kuna watanzania tena vijana wanashiriki kutishia kupoteza vijana wenzao. Honestly hili limenishangaza kidogo,”amesema.