MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umelitaka Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Uhamiaje kutoa taarifa ya alipo Mwanaharakati Godlisten Malisa, na anashikiliwa tuhuma gani.Anaripoti Faki sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Wito huo umetolewa na Onesmo Olengurumwa Mratibu wa Kitaifa THRDC, ambapo ameeleza kuwa ufuatiliaji wao unaonesha mashaka kwa kuwa simu za Malisa hazipatikani na vyombo hivyo havijatoa taarifa ya wapi alipo.
“Mtandao wa Watetezi wa Hainatoa wito kwa Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji kutoa mara moja taarifa rasmi kuhusu mahali Malisa anaposhikiliwa, sababu na msingi wa kisheria wa hatua hiyo,” imeeleza taarifa ya Olengurumwa.
Amesema kuwa mamlaka zihakikishe usalama wake na zimwezeshe kuwasiliana na familia yake pamoja na kuonana na mawakili wake bila kizuizi.
Taarifa za kushikiliwa kwa Malisa zimepatikana jana tarehe 31 Agosti 2026 ambapo inadaiwa kushikiliwa katika mpaka wa Tanzania na Kenya (Namanga).
Malisa alikuwa akirejea nchini akitokea Marekani kupitia Nairobi, Kenya.Kwa mujibu wa taarifa za awali, Malisa aliwasili Namanga majira ya saa tisa alasiri na kuwasilisha hati yake ya kusafiria kwa maafisa wa Uhamiaji. Baada ya kusubiri kwa saa kadhaa, aliondolewa eneo hilo na kupelekwa Kituo cha Polisi Longido.
Baadaye gari hilo liliondoka kuelekea Arusha, huku simu zake zikiwa hazipatikani. Hadi wakati wa kutoa taarifa hii, mamlaka husika hazijatoa uthibitisho rasmi wa mahali alipo wala sababu za kushikiliwa kwake.
Malisa ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Gifted Heart Foundation (GH Foundation), shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi nchini Tanzania, ikiwemo katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na magonjwa yasiyoambukiza.
MwanaHALISI Digital itakupa muendelezo wa Tarifa hizi hapo baadaye.