SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, limetangaza kuwa bei za vyakula duniani zimeongezeka kwa mwezi wa tatu mfululizo mwezi Aprili. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Ongezeko hilo limechangiwa zaidi na kupanda kwa bei ya mafuta ya mimea kufuatia usumbufu uliosababishwa na vita vya Iran.
Kielezo cha Bei za Chakula cha FAO, ambacho hupima mabadiliko ya bei za bidhaa mbalimbali za chakula katika masoko ya kimataifa, kiliongezeka kwa asilimia 1.6 mwezi Aprili.
Baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28 na kuzuka kwa vita, shughuli za meli katika Mlango wa Hormuz zilianza kudhibitiwa, na licha ya kusitishwa kwa mapigano, vizuizi hivyo bado havijaondolewa.
Mlango wa Hormuz ni njia muhimu inayopitisha asilimia 20 ya mafuta na gesi kimiminika duniani.
Wakati huo huo, karibu theluthi moja ya biashara ya kimataifa ya mbolea za kemikali na malighafi zake hupitia katika Mlango wa Hormuz. Kufungwa kwa njia hiyo ya majini kumeongeza shinikizo katika sekta ya kilimo na uzalishaji wa chakula duniani.
Bei ya mbolea za kemikali imeongezeka kwa asilimia 80 tangu kuanza kwa vita hivyo.