SHIRIKA la Kimataifa la Masuala ya Bahari la Umoja wa Mataifa, International Maritime Organization (IMO), limesema takribani meli 1,500 pamoja na mabaharia zaidi ya 20,000 wamekwama katika eneo la Ghuba ya Uajemi kufuatia vikwazo vilivyowekwa na Iran katika Mlango wa Hormuz.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza jana Alhamisi 7 Mei 2026 akiwa nchini Panama wakati wa mkutano wa bahari wa Inter-American Maritime Summit, Katibu Mkuu wa IMO, Arsenio Dominguez, amesema hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa usafiri wa baharini pamoja na biashara ya kimataifa.
Mvutano huo ulianza 28 Februari baada ya Israel na United States kufanya mashambulizi dhidi ya Iran, hatua iliyosababisha Tehran kujibu kwa mashambulizi katika maeneo mbalimbali na hatimaye kuzuia upitishaji wa meli kupitia Mlango wa Hormuz, ambao ni moja ya njia muhimu zaidi za biashara duniani.
Dominguez amesema mabaharia hao wamejikuta wakikwama bila hatia huku wakibeba mzigo wa mgogoro wa kisiasa usiowahusu moja kwa moja.
“Mabaharia hawa ni watu wa kawaida wanaotekeleza majukumu yao, lakini sasa wanateseka kutokana na hali ya kisiasa iliyo nje ya uwezo wao,” amesema.
Katika hatua nyingine, Marekani ilitangaza operesheni ya kusindikiza meli katika eneo hilo Jumatatu, lakini ikafuta tangazo hilo siku moja baadaye bila kutoa maelezo ya kina kuhusu uamuzi huo.