MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umezitaka serikali za Tanzania na Kenya kuharakisha uchunguzi wa kupotea kwa mwanaharakati Mtanzania Twaha Mwaipaya, anayedaiwa kutekwa nchini Kenya.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es salaam …  (endelea)
Umetaka pia familia yake ipewe taarifa sahihi kuhusu alipo na hali yake ya usalama.
Katika taarifa iliyotolewa leo tarehe 26 Oktoba, 2026 na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC Wakili Onesmo Olengurumwa, imesema imepokea kwa masikitiko taarifa za kupotea kwa Mwaipaya, ambaye kwa mujibu wa taarifa za awali, anadaiwa kutekwa Jumapili, 25 Oktoba 2026, nje kidogo ya jiji la Nairobi.
Mtandao huo umesisitiza kuwa mazingira ya tukio hilo yanahitaji uchunguzi wa haraka, huru na wa kina ili kubaini alipo Mwaipaya, hali yake ya usalama na watu waliohusika, iwapo itathibitika kuwa alitekwa.
Kwa mujibu wa mtandao huo, ushirikiano wa mamlaka za Tanzania na Kenya ni muhimu katika kuhakikisha ukweli wa tukio hilo unafahamika na familia inapata taarifa za kuaminika kwa wakati.
“Kwa kuwa tukio hilo limeripotiwa kutokea nchini Kenya, THRDC imesema mamlaka za nchi hiyo zina wajibu wa kuchunguza mazingira ya kupotea kwa Mwaipaya na kuhakikisha haki zake za msingi zinalindwa”
Mtandao huo umetaja Ibara za 21(1), 26 na 29 za Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, zinazohusu masuala ya haki za msingi, wajibu wa kuheshimu Katiba na sheria, pamoja na haki ya kuishi, uhuru na usalama wa mtu.
Aidha, THRDC imesema iwapo itabainika kuwa Mwaipaya amekamatwa au anashikiliwa na mamlaka za serikali, haki zinazotambuliwa chini ya Ibara za 49 na 51 za Katiba ya Kenya zinapaswa kuzingatiwa.
Haki hizo zinajumuisha ulinzi wa kisheria kwa watu waliokamatwa au kuwekwa kizuizini, pamoja na uwezekano wa kuomba amri ya habeas corpus kwa mujibu wa sheria.
THRDC imetaka uchunguzi ufanyike kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotumika ili ukweli ujulikane na wahusika wawajibishwe iwapo itathibitika kuwa kosa la jinai limetendeka.
Kwa upande wa Tanzania, THRDC imeitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia ubalozi wake jijini Nairobi, kuongeza juhudi za kidiplomasia katika kufuatilia suala hilo.
Mtandao huo umesema ulinzi na usaidizi kwa Watanzania walioko nje ya nchi ni miongoni mwa masuala yanayohitaji ufuatiliaji wa serikali kwa kuzingatia sheria za ndani na mikataba ya kimataifa.
Katika hoja hiyo, THRDC imetaja Mkataba wa Vienna wa Mahusiano ya Kidiplomasia wa mwaka 1961 na Mkataba wa Vienna wa Mahusiano ya Kibalozi wa mwaka 1963, inayoweka misingi ya mahusiano ya kidiplomasia na kibalozi.
Mtandao huo umesisitiza kuwa serikali za Tanzania na Kenya zinapaswa kushirikiana kwa karibu katika kufuatilia tukio hilo na kutoa taarifa sahihi kwa familia ya Mwaipaya na umma.
THRDC imewataka wanaharakati na wanasiasa kutathmini hatari za kiusalama, kuweka mifumo ya mawasiliano ya dharura na kuripoti vitisho kupitia njia salama.
Mwisho.