SHIRIKA la Viwango la Taifa (TBS), limewataka wajasiliamali wadogo na kati, kujitokeza kusajili biashara zao, kwa lengo la kupata vyeti vya ubora, ili kuzifanya biashara zao, “kuingia kwenye soko la ushindani la ndani, kikanda na kimataifa.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Hayo yameelezwa leo Jumanne na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Ashura Katunzi, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Dk. Katunzi, jumla ya vyeti na leseni za ubora 3,940 vimetolewa kwa wazalishaji, miongoni mwao wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683. Amesema, vyeti hivyo, hutolewa bila malipo.
Amesema, “Serikali imekuwa ikitenga zaidi ya Sh. 300 milioni kila mwaka, kwa madhumuni ya kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.
“Leseni hizi zimesaidia wazalishaji kuweza kuzalisha bidhaa bora, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao kuweza kuaminika sokoni na kufanya biashara nje ya mipaka ya Tanzania, hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa,” amefafanua.
Ameongeza, “Shirika limeendelea na huduma za usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo, ili kuendelea kulinda afya za walaji ambapo jumla ya bidhaa 9,731 na maeneo 80,836 yalisajiliwa.”
Aidha, Dk. Katunzi amesema, katika kuimarisha ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia nchini kutoka nchi za nje, TBS huhakiki ubora wa bidhaa na magari yaliyotumika kabla ya kusafirishwa kuja nchini. Amesema, jumla ya magari 249,386 yalikaguliwa kabla ya kuingizwa nchini.
Amesema, katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita, jumla ya shehena za bidhaa 183,186 zilikaguliwa kabla ya kuingia nchini kupitia mfumo wa Pre-Shipment to Conformity (PVoC) na shehena za bidhaa 426,842 zilikaguliwa baada ya kufika nchini kupitia mfumo wa Destination Inspection (DI).
Anasema, ukaguzi huo, umelenga kuiepusha nchi kuwa jalala la bidhaa duni pamoja na kulinda afya, usalama na mazingira ya watumiaji.
Kwa upande wa mafunzo, Dk. Katunzi amesema, TBS imeweza kutoa mafunzo kwa jumla ya wadau 6824 wakiwemo wazalishaji wa bidhaa za viwandani na wasindikaji.
Amesema, mafunzo hayo yalihusu dhana nzima ya viwango na ubora ambayo yatawawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango na kuwezesha wahusika kupata uelewa mpana kwenye masuala ya udhibiti ubora, hivyo kuwaandaa kuhimili ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Vilevile, TBS imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza uelewa juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora.
Amezitaja hjia hizo kuwa pamoja na kuanzisha kliniki ya viwango ambayo inaendelea katika maeneo mbalimbali; pamoja na kushiriki katika makongamano, maonesho, warsha na semina; kuandaa mikutano na wadau wa masuala ya viwango, kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya ubora na usalama; na kuendesha kampeni za elimu kwa umma katika ngazi za wilaya.
Akizungumzia kuongeza ufanisi wa maabara, Dk. Katunzi amesema, TBS ina jumla ya maabara 14 na zote zimeweza kupata ithibati za umahiri, ambapo maabara hizo zimehakikiwa na kupatiwa vyeti vya ithibati ya umahiri wa kimataifa.
“Hatua hiyo inamaanisha kuwa majibu ya sampuli kutoka katika maabara hizo yanaaminika na kukubalika popote duniani na hivyo kurahisisha biashara ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu,” amefafanua.
Amesema, katika kipindi hicho TBS imeweza kupima sampuli zaidi ya 188,952 na kufanyia ugezi vifaa 54,396 jambo lililosaidia kuhakikisha soko linakuwa na bidhaa zenye ubora.
Amesema, maabara hizo zina mashine za kisasa zinazoweza kupata majibu kwa wakati na sahihi, na kwamba Serikali imeweza kutumia kiasi kisichopungua Sh. 12.9 bilioni kununua mashine hizo.
Mbali na uwekezaji huo, Serikali imetumia zaidi ya Sh. 9.8 bilioni kwa ajili ya kuimarisha ofisi tisa za kanda (Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Pwani na Geita pamoja na ofisi za mipakani (Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea, Namanga, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Mwanza na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.
Maeneo mengine yaliyotajwa ni Sirari, Kabanga, Rusumo, Mutukula, Kasesya, Bandari ya Bagamoyo, bandari ya Mbweni, bandari ya Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Bandari ya Tanga, pamoja na kuongeza ofisi mpya za kanda, wafanyakazi na vitendea kazi.