KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Idara ya Oganaizesheni, Paul Chacha, ametangaza hadharani kuwa vyombo vyote vya dola na viongozi wa serikali ni mali halali ya CCM. Anaandika Salehe Mohamed … (endelea).
Kwa amelezo yake CCM ndicho kinateua mawaziri, mkuu wa majeshi, mkuu wa jeshi la polisi, magereza, usalama wa taifa, wakurugenzi wa halimashauri, wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya.
Kauli yake ilikuwa ni majibu kwa wakosoaji na vyama vya upinzani vinavyohoji umiliki wa dola na utaratibu wa CCM kuwasomba wananchi kwenye mikutano yao.
Baada ya kauli hiyo nimeona baadhi ya watu wakimparura na kumtaka aombe radhi. Binafsi siwaelewi na sitawaelewa wanaomkosoa Chacha ambaye ni miongoni mwa viongozi wachache ndani ya CCM kusema kikilichopo bila hofu na kwa ujasiri
Hivi Chacha amesema kipi kipya kisichojulikana hadi kiwafanye watu watake kutoana macho? Alichokisema si ndicho maisha ya kila siku na kinawachochea watu kudai Katiba mpya kila kukicha?
Si ndiyo maana watu wanataka Rais apungiziwe madaraka ya kuteua?
Chacha amerejesha kumbukumbu zangu hadi tarehe 20 Machi, 2020, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ali, alikiri chama chake kinatumia dola kuhakikisha kinabaki madarakani.
Kwa maelezo yake kama chama chochote kinachoongoza serikali kitashindwa kutumia dola kubaki madarakani, utakuwa uzembe wa chama chenyewe. Anasema CCM imekuwa ikitumia dola kujihakikishia ushindi wakati wa uchaguzi na mwaka huu wamepanga “kuitumia dola kweli kweli”.
“Ukishakuwa chama tawala, kuna dhana inaitwa nafuu ya mwenye madaraka. Ukishindwa kutumia nafuu hiyo, utakuwa kama KANU (chama tawala cha zamani cha Kenya), iliposhindwa kutumia nafuu hiyo, haikuwahi kurudi madarakani au UNIP ya Zambia.
“Unashika dola halafu unatumia dola kubaki madarakani. Akitokea mtu mwenye busara zaidi, akakwambia usitumie dola, ukamsikiliza, siku ukishatoka hurudi. Aliye na dola anatumia dola hiyo kubaki madarakani. Ukweli hata Chadema ikiingia madarakani, kuiondoa kwenye dola itakuwa ni uzembe wake, kwa sababu ana nafuu na faida ya kuwa na dola.”
Hebu nirudi kwa ndugu yangu Chacha, kipi cha ajabu kwani ni uongo viongozi hao wote hawateuliwi na hawajibiki kwa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM?
Kumlaumu Chacha kwa kauli yake ni kutofikiri kisawasawa, mara ngapi tumewasikia wana-CCM wenyewe wakilalamikia mkono wa vyombo vya dola kwenye mchujo au chaguzi zao?
Kama Chacha hayuko sahihi, kwa nini wakuu wa vyombo hivyo wamekaa kimya hadi sasa wakishuhudia minyukano inayozidisha utata wa kisiasa ndani ya nchini.
Si tuliona Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), lilivyojitokeza kueleza haliko pamoja na wale waliokuwa wakifanya maandamano na vurugu katika uchaguzi mkuu uliopita, mbona hivi sasa limenyamaza kimya?

Tuwe wakweli ni mkuu gani wa chombo cha dola anayekitaka bibarua chake anaweza kufanya tofauti na anavyotaka aliyemteua?
Kwa muda mrefu viongozi wa CCM na wanachama wao wanajua wanavyovitumia na kumiliki vyombo vya dola ndiyo maana walishtuka waliposikia kauli ya Rais Jakaya Kikwete alipowaambia ‘wasitegemee polisi kujibu hoja za wapinzani.’
Kikwete alionekana akiwageuka wenzake lakini ukweli alikuwa akitoa ujumbe kwa pande zote mbili. Kwa polisi kuwa wafanye kazi zao bila kuwapendelea CCM na kuwaonea wapinzani. Kwa CCM wajifunze kujitegemea na kupambana na vita vyao bila kutegemea polisi.
Mmiliki wa mali ndiye mwenye kuamua namna ya kutumia mali yake. Nategemea kuelekea mchakato wa Katiba mpya tutamulika maeneo yote yenye utata yanayofifisha demokrasia.
Tanzania ilipokubali mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 ilitegemewa mifumo, miongozo, sheria na kanuni mbalimbali zingebadilishwa ziendane na mfumo huo.
Ibara va 3(1) va Katiba inaeleza kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vvama vingi. Ibara ya 4 inaainisha namna mamlaka va dola yanavyotakiwa kutekelezwa kupitia vyombo vya Serikali.
lbara ya 8 inaweka msingi thabiti kwamba mamlaka na nguvu zote za Serikali zinatokana na wananchi na Serikali inawajibika kwa wananchi.
Kisheria, kitu kinapokuwa mali ya mtu au taasisi mwenye mali ndiye mwenye haki ya kukitumia na kukiamulia matumizi yake Katika misingi ya haki Serikali na vyombo vyake havipaswi kuwa mali ya chama cha siasa kilichopo madarakani.
Serikali na vyombo vyake vinapaswa kuwa ni mali ya wananchi si mali ya CCM au chama chochote kitakachoingia madarakani. Katiba imetoa ulinzi maalumu dhidi ya kuchanganya vyombo vya ulinzi na siasa. Ibara ya 147(3) inakataza mfanyakazi wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwa mwanachama wa chama cha siasa (isipokuwa haki yake ya kupiga kura).
Sina hakika kwa mazingira tuliyonayo na kwa hawa wanaojisifu kumiliki vyombo vya dola kuna mpinzani anaweza kupenya kwenye sanduku la kura hata kama wananchi watamchagua. Haki kwa mpinzani haiwezi kutendeka akikabiliana na mmliki.

Kwa Taifa linalojivunia miaka 60 ya uhuru na kwa chama kinachojivunia miaka 49 tangu kuanzishwa kwake, kauli ya Chacha haipaswi kuachwa ipite hivi hivi kwa kuwa inaharibu umoja na mshikamano uliopo kwenye jamii. Inazidisha ufa wa kisiasa.
Nakumbuka waziri mkuu mstaafu Joseph Warioba alionya vyombo vya dola visijiingize au visihusishwe na siasa. Kwa maelezo yake JWTZ ndicho chombo pekee cha dola kinachoaminiwa na wananchi hivyo akasihi kisijiingize au kuingizwa kwenye siasa.
Naamini tusipochunga ndimi zetu tutauvuruga mchakato wa Katiba mpya na utakwama kama ilivyokuwa mwaka 2014. Tusipochunga ndimi zetu tutashuhudia kesi nyingi za uhaini na ugaidi zikiwahusu wapinzani.
Itashindikana vipi wapinzani kujaa vituo vya polisi na magerezani wakati sote tunajua vyombo vyote vya ulinzi na usalama ni mali ya CCM na vinaweza kutumika kulinda waliopo madarakani?
Tunajua Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ni mali ya CCM. Hata viongozi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni mali ya CCM.
Kama hatukumuelewa Kikwete, Dk. Bashiru hivi sasa tunawezaje kumuelewa Chacha aliyetuambia uhalisia tunaoujua?, Labda kama tunataka kumlaumu kusema wakati usiofaa?
Mwisho.