MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeeleza kusikitishwa na kukamatwa kwa wafanyakazi watatu wa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC), shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi jijini Arusha.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakili na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC Onesmo Olengurumwa, leo 7 Oktoba 2026,imesema wafanyakazi hao ni Thadeus Clamian, Nangei Meitaya na Ezekiel Kishau, ambao walikamatwa na Polisi 6 Oktoba 2026, pamoja na Salangat Makko, ambaye si mfanyakazi wa PWC.
THRDC imesema kwa mujibu wa taarifa ilizopokea, watu hao wanatuhumiwa kupanga maandamano yaliyolenga wabunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) waliopo nchini.
Aidha Mtandao huo umedai kuwa baada ya kukamatwa kwa wafanyakazi hao, Polisi wameendelea kuwatafuta wafanyakazi wengine wa PWC, huku baadhi yao wakifuatiliwa hadi majumbani kwao nyakati tofauti, ikiwamo usiku.
THRDC imeongeza kuwa 5 Oktoba 2026, Polisi walifanya upekuzi katika moja ya makazi ya mfanyakazi wa PWC wakati wa usiku, bila kueleza sababu za upekuzi huo.
Tukio hilo, kwa mujibu wa THRDC, limeibua hofu miongoni mwa wafanyakazi wa PWC, familia zao na mashirika mengine ya kiraia jijini Arusha.
Katika hatua nyingine, THRDC imesema imewaelekeza mawakili Simon Mbwambo na Ally Mhyellah kufuatilia suala hilo katika Kituo cha Polisi Kati, Arusha, kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa waliokamatwa.
Aidha, THRDC imesema Wakili Lairumbe anaendelea kufuatilia suala hilo kwa niaba ya PWC.THRDC imeitaka Jeshi la Polisi kuwaachia wafanyakazi hao bila masharti, ikisema hakuna shirika lolote mwanachama wa THRDC linaloratibu maandamano hayo.
Pia, mtandao huo umelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wafanyakazi wote waliokamatwa wanapewa fursa ya kuwasiliana na mawakili wao pamoja na familia zao.