DK. Azaveli Lwaitama, Mwanazuoni na mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, amesema kuwa kitendo cha watu kutoamini mifumo ya haki na kuwepo kwa matumizi ya nguvu kwenye utawala wa sheria kunaweza kuharibu mwenendo wa taifa.Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Mwanazuoni huyo akizungumza na MwanaHALISI Digital, amesema kuwa jambo jingine linaloyumbisha mifumo hiyo ni kuwepo kwa manufaa ya wachache badala ya umma.
“Ukiwa unatengeneza mazingira ya watu kutoiamini mifumo ya kutenda haki unawatengenezea watu waamini kila mtu na lake na mwenye nguvu mpishe,” amesema Dk. Lwaitama.
“Nchi yenye watu wenye kufikiria kila mtu na lake mwenye nguvu mpishe haiwezi kuwa na usalama huko mbele ya safari …ndio inakuwa hata kuingia kwenye nafasi ya uongozi kunakuwa ni kuuana kutishana kwa sababu kwanza wanaonufaika ni wachache, wakishanufaika hawataki mtu yeyote awaondoe pale walipo halafu mifumo yenyewe sio haki.
Ameongeza kuwa “Mahakama haijitegemei, watendaji kama polisi hawafuati sheria wanafuata wewe ni nani ni mtoto wa nani, una nini sasa nchi ya namna ile haiwezi kuwa na usalama mbele ya safari”.
Dk. Lwaitama amesema kuwa mfumo wa kijitawala utaharibiwa endapo kila mtu akijisikia yeye ni sehemu ya maamuzi tunatengeneza kizazi cha kila mtu na lake mwenye nguvu mpishe.