Jamii Africa kwa kushirikiana na kampuni ya kiteknolojia kutoka Canada VIAMO, wamezindua teknolojia ya Akili Unde (AI) ya sauti inayowawezesha wananchi kupata taarifa na majibu ya maswali mbalimbali bila kuhitaji intaneti wala kutumia simu janja.Anaripoti mwandishi wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Uzinduzi wa teknolojia hiyo umefanyika leo, Septemba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla iliyohudhuriwa na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, ambaye alikuwa mgeni rasmi, wadau wa habari, asasi za kiraia na wadau wa teknolojia.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkuu wa Programu kutoka Jamii Africa, Ziada Seukindo, amesema lengo la teknolojia hiyo ni kujenga jamii yenye upatikanaji wa taarifa sahihi na zinazoweza kuaminika ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao ya kila siku.
Amesema kupitia mradi huo wameanzisha mfumo unaoitwa AVA (Ask Viamo Anything) unaomwezesha mtumiaji kupiga simu na kuuliza swali kwa kutumia sauti, kisha kupata jibu kutoka kwenye mfumo wa AI.
Kwa mujibu wa Seukindo, huduma hiyo kwa sasa inapatikana kwa watumiaji wa mtandao wa Vodacom kupitia namba 0901760321, huku mtumiaji akiwa hahitaji kuwa na simu janja wala kifurushi cha intaneti ili kuitumia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo, amesema uzinduzi wa AVA unalenga kupunguza pengo la upatikanaji wa taarifa kati ya wananchi wanaotumia simu janja na wale ambao hawana uwezo wa kutumia teknolojia hizo.

Melo amesema teknolojia hiyo itawasaidia wananchi, hususan wale wanaoishi mijini na vijijini, kupata taarifa kupitia teknolojia rahisi ya simu za kawaida, hivyo kuwawezesha kunufaika na fursa za kidijitali bila vikwazo vya umiliki wa simu janja au upatikanaji wa intaneti.
Amesema Jamii Africa inalenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo vyombo vya habari, serikali, asasi za kiraia, kampuni za simu pamoja na watengenezaji wa maudhui.
Kwa upande wake, Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, amepongeza Jamii Africa na Viamo kwa kuja na teknolojia hiyo akisema ina uwezo wa kusaidia jamii kupata taarifa sahihi kwa kutumia nyenzo za kidijitali zinazopatikana kwa urahisi.
Amesema Canada itaendelea kutoa ushirikiano katika jitihada zinazolenga kutumia teknolojia na ubunifu wa kidijitali kuboresha upatikanaji wa taarifa na huduma kwa wananchi.
Teknolojia hiyo imezinduliwa wakati ambapo matumizi ya Akili Unde yanaendelea kuongezeka katika sekta mbalimbali, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha teknolojia hizo zinawafikia watu wote, wakiwemo wale ambao bado hawana simu janja au upatikanaji wa uhakika wa intaneti.