CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, linapaswa kuvunjwa na kuundwa upya. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
“Jeshi la Polisi nchini, limepoteza hadhi na sifa ya kuwa chombo cha kulinda usalama wa raia na mali zao,” ameeleza Dk. Rugemeleza Nshala, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, leo Jumamosi, tarehe 19 Septemba 2026.
Akaongeza, “Jeshi la Polisi, limekuwa wakala wa chama kilichoko Ikulu. Hivyo haliwezi tena kuwa chombo kinachoaminika mbele ya wananchi waliowengi.”
Kwa mujibu wake, jeshi hilo, limepoteza sifa ya kuwa taasisi ya umma. hakufafanua.
Bali matukio kadhaa mbalimbali za huko nyuma, zinatuhumu polisi, kushiriki au kunyamazia vitendo vya uhalifu, ikiwamo vitendo vya utekaji na mauaji ya raia.
Dk. Nshala alitoa kauli hiyo, wakati akitoa msimamo wa Kamati Kuu (CC) ya chama chake, makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Alisema, kuvunjwa kwa Jeshi la Polisi, ni takwa lililotolewa na Tume ya Rais ya Haki Jinai, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo pamoja na mengine, ilipendekeza jeshi hilo kuvunjwa na kuundwa upya.
Hata hivyo, Dk. Nshala amesema, pendekezo hilo, halijufanyiwa kazi kwa kuwa linakweenda kinyume na matamanio ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka kutumia Polisi kubaki madarakani.
Tume ya Rais ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini, anayoitaja Dk. Nshala, kwamba ilipendekeza kuvunjwa kwa Jeshi la Polisi, iliongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman Chande.
Rais Samia alipokea ripoti ya tume hii, tarehe 15 Julai 2023, ikiwa na mapendekezo 333 kuhusu maboresho ya mfumo mzima wa haki jinai nchini na kuahidi kuyafanyia kazi.
Baadhi ya mapendekezo kuhusu Jeshi la Polisi, yake yalikuwa na uzito mkubwa. Yalilenga kulibadilisha Jeshi la Polisi kutoka mfumo unaosisitiza zaidi kukamata na kupeleleza baada ya uhalifu kutokea, kwenda kwenye mfumo wa kuzuia uhalifu, kuheshimu haki na kuwajibika kwa wananchi.
Tume ilipendekeza kuanzishwa kwa National Bureau of Investigation (NBI) – chombo huru cha uchunguzi wa makosa ya jinai – kitakachotenganishwa na Jeshi la Polisi.
Kwa maana hiyo, kazi ya polisi ya kulinda usalama na kazi ya uchunguzi wa jinai zisitawaliwe na mlolongo uleule wa uongozi.
Mapendekezo haya yameendelea kuwa kwenye mjadala wa sera Tanzania.
Mathalani, Ilani ya CCM ya 2025–2030 iliweka pia pendekezo la kuanzishwa kwa NBI huru kuchukua nafasi ya baadhi ya kazi zinazofanywa sasa na Idara ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai (CID), lakini pendekezo hilo, halijafanyiwa kazi karibu mwaka mmoja tangu chama hicho, kitangazwe kuwa mshindi wa uchaguzi.
Jaji Chande mwenyewe alisema Tume iligundua watu wengi kuwekwa mahabusu kwa muda mrefu kinyume cha sheria.
Akapendekeza kuwepo mfumo madhubuti wa kushughulikia malalamiko dhidi ya polisi, hususan pale maafisa wanapotuhumiwa kutumia vibaya mamlaka, kuvunja sheria au kukiuka haki za wananchi.
Mpaka sasa, hakuna lililofanyiwa kazi.