MAHAKAMA Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam inatarajia kusikiliza mawasilisho ya mwisho kwenye kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) siku ya tarehe 23 Septemba 2026.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Mahakama imetoa uamuzi huo baada ya Lissu kueleza kuwa amehitimisha utetezi wake na kuiomba mahakama ipange tarehe maalum kwa ajili ya kusikiliza hoja za mwisho (Final Submissions) za pande zote mbili.
Upande wa mashtaka umeunga mkono ombi hilo, lakini ukaomba ufafanuzi kuhusu namna hoja hizo zitakavyowasilishwa, ikiwa ni kwa njia ya mdomo au maandishi.
Akijibu, Lissu amesisitiza kuwa hoja za mwisho zitolewe kwa njia ya mdomo, akieleza kuwa akiwa gerezani hana fursa ya kupata baadhi ya zana na nyenzo zinazopatikana kwa upande wa Jamhuri.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama imeahirisha shauri hilo na kupanga kusikiliza hoja za mwisho kwa njia ya mdomo Jumatano 23 Septemba 2026.