Rais Samia Suluhu Hassan
MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, nchini Tanzania, imetupa ombi la Tundu Lissu, Kiongozi wa Upinzani nchini, kuwaita mahakamani hapo Rais Samia Suluhu Hassan; aliyekuwa makamu wake wa rais, Philip Mpango; aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkurugenzi wa sasa wa Usalama wa Taifa (TISS), Suleiman Abubakar Mombo. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).
Akisoma uamuzi mdogo katika kesi ya Uhaini, inayomkabili mwenyekiti huyo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Jaji Dunstan Ndunguru alisema, siyo sahihi kuwaita mashahidi hao kwa madhumuni ya kuthibitisha iwapo walitishika au hawakutishika kutokana na kauli zinazolalamikiwa katika shauri hilo.
Alisema, madai yaliyopo mahakamani, yanahusu “matamshi ya mshitakiwa yalikuwa na nia ya kuitisha serikali.”
Alisema, “….katika kuamua kama mashahidi hao waitwe au la, Mahakama imezingatia hoja ya msingi, kwamba iwapo ushahidi wao una umuhimu (relevance) au la katika shauri lililopo. Jukumu la kuthibitisha mashitaka ni la upande wa Jamhuri na si la upande wa utetezi, kwa kuwa mashauri ya jinai huanzishwa na upande wa mashtaka.”
Akaongeza, “Hati ya mashitaka inaeleza kwamba mshitakiwa anatuhumiwa kuwa na nia fulani ya kutenda kosa, na si kwamba aliwatisha viongozi wa serikali moja kwa moja.”
Kwa msingi huo, Jaji Ndunguru alisema, Mahakama imeona mashahidi hao wanne – Rais Samia, Dk. Mpango na Majaliwa – hawastahili kuja mahakamani, kueleza kama walitishika kama ambavyo mshitakiwa anavyotaka.”
Akizungumzia sababu za kutomuita Mkurugenzi Mkuu wa TISS, kutoa ushahidi, Jaji Ndunguru alisema, Mahakama imeirejea kesi ya Khatibu Gandhi, ambayo ilitumiwa na mshtakiwa katika hoja zake. Alisema, katika shauri hilo, Mkurugenzi wa TISS, alikuwa shahidi wa upande wa mashitaka na siyo upande wa utetezi kama inavyotakiwa katika kesi ya sasa.
Kesi dhidi ya Lissu, inasikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Ndunguru. Majaji wengine wanaosikiliza shauri hilo, ni Ferdinand Kiwonde na James Karayemaha.
Kabla ya kufikia hitimisho hilo, Jaji Ndunguru alisema, mtakumbuka kwamba tarehe 21 Agosti mwaka huu, Mahakama hii ilitoa uamuzi mdogo kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu na ikamweleza kuwa ana haki ya kuleta mashahidi wake.
Katika orodha ya mashahidi aliowataja, walikuwemo Samia Suluhu Hassan,
Dk. Philip Mpango, Kassim Majaliwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Jenerali John Jacob Mkunda, Mkuu wa Majeshi, Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai.
Mashahidi wengine, walikuwa John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema; Amani Golugwa, naibu katibu mkuu; John Heche, makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara na Brenda Rupia, mkurugenzi wa mawasiliano.
Alisema, “Baada ya kuwasilisha orodha hiyo, mshtakiwa aliiomba Mahakama itoe wito kwa mashahidi hao ili waweze kufika kutoa ushahidi. Lakini upande wa mashitaka uliweka pingamizi chini ya Kifungu cha 218(1) na Kifungu cha 304 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Alisema, upande wa mashtaka uliwasilisha hoja sita za kupinga mashahidi hao. Kwamba, wakati shauri likiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mashahidi hao hawakuwa wametajwa, hivyo hawakustahili kuitwa baadaye, ingawa mshtakiwa aliwataja mashahidi hao shauri lilipofika Mahakama Kuu, hakuwataja katika hatua za awali.
Aidha, Wakili wa Serikali alidai kwamba ushahidi wa baadhi ya mashahidi hao, hususan Samia na Dk. Mpango, haukuwa na uhusiano wa moja kwa moja na masuala yanayobishaniwa kwenye kesi hiyo.
Kwamba, baadhi ya mashahidi waliopendekezwa ni watumishi wa umma, na kwamba kuwaita kulionekana kuwa ni juhudi za kuwauliza maswali ya dodoso kuhusu ushahidi uliokwisha kutolewa, hususan iwapo walitishika au hawakutishika kutokana na kauli zinazodaiwa kutolewa na mshtakiwa.
Hoja nyingine ya upande wa mashitaka ilitokana na Kifungu cha 9 cha Sheria ya Kinga ya Rais, ambacho kinaeleza kwamba Rais si shahidi anayelazimika kuitwa kutoa ushahidi mahakamani.
Baada ya kusikiliza hoja za mashtaka, mshtakiwa alijibu kwa kuomba Mahakama itoe wito kwa mashahidi wote aliowataja, akisema ni haki yake ya kikatiba kuita mashahidi anaowaona kuwa muhimu katika utetezi wake.
Alieleza kwamba Mahakama hii ilishapokea orodha ya mashahidi hao wakati shauri likiendelea, licha ya kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikuwa imekataa ombi hilo. Aidha, alisema kuwa ingawa baadhi yao ni maafisa wa Serikali, bado wanawajibika kutoa ushahidi endapo wataitwa na Mahakama.
Mshtakiwa alisisitiza kuwa hakuna sheria inayowazuia viongozi hao kupewa wito wa Mahakama. Alisema, ushahidi wao una umuhimu mkubwa kwa sababu shitaka linalomkabili linahusu kutishia Serikali, na kwamba Rais akiwa Mkuu wa Nchi anahusika moja kwa moja na suala hilo.
Aidha, Lissu alisema, mashahidi hao wangeisaidia Mahakama kufahamu vizuri iwapo tukio linalodaiwa lilitokea na mazingira yake.
Kuhusu hoja ya kwamba baadhi ya mashahidi walikuwa wamewakilishwa tayari kupitia mashahidi wengine walioitwa na upande wa mashtaka, mshtakiwa alisema sheria haisemi kwamba jambo hilo linamzuia kuwaita mashahidi hao.
Upande wa mashtaka ulipopewa nafasi ya kujibu hoja za mshtakiwa, ulisisitiza msimamo wake wa awali.
Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Mahakama ilijielekeza kwenye suala la msingi la kuamua iwapo pingamizi hilo lina mashiko au la.
Mahakama imebaini kwamba katika mwenendo wa shauri lililokuwa Mahakama ya Kisutu, ni kweli Mahakama hiyo haikuwa imewaorodhesha, lakini mshitakiwa aliwataja mashahidi hao.
Kwa hiyo, Mahakama imeona kwamba hatua zilizofanyika baadaye haziwezi kurekebisha makosa au mapungufu yaliyotokea katika hatua za awali za shauri. Kwa msingi huo, Mahakama imekubaliana na hoja hiyo ya Jamhuri.
Kutokana na sababu hiyo, Mahakama imeona kuwa si sahihi kutoa wito kwa mashahidi hao ili waje kujibu swali la iwapo walitishika au hawakutishika.
Hata hivyo, Jaji Ndunguru alisema, Mahakama imekubali IGP, DCI na Mkuu wa Majeshi kutoa ushahidi katika kesi hii.
Alisema, Mahakama imeona kuwa mashahidi hao wana umuhimu katika shauri hili na ushahidi wao unaweza kusaidia katika kuibainishia Mahakama baadhi ya masuala yanayohusika katika kesi hiyo.