SHAURI la ugaidi linalomkabili mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Melikisedeki Kaijage, limeahirishwa hadi 19 Agosti 2026 baada ya kutajwa leo 5 Agosti 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Shauri hilo lilitajwa mbele ya Hakimu Mfawidhi, Zabibu Mpangule, ambapo ilielezwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kulisikiliza, bali jukumu lake ni kuhakikisha faili la shauri linakamilika kabla ya kupelekwa katika mahakama yenye mamlaka ya kulisikiliza.
Mahakama imeiagiza Jamhuri kuharakisha uchunguzi wa shauri hilo, ikieleza kuwa kutokana na mtuhumiwa kuwa mtumishi wa umma, ni vyema uchunguzi ukakamilika mapema ili endapo hana hatia aweze kurejea kutekeleza majukumu yake.
Dk.Kaijage alifikishwa mahakamani huku akiendelea kushikiliwa rumande, ambapo uchunguzi wa shauri hilo bado unaendelea.
Dk. Kaijage alikamatwa 8 Julai 2026 na anakabiliwa na tuhuma za kuhamasisha maandamano.