SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar sasa italazimika kueleza kwa ufasaha ni takwimu ipi iliyo sahihi kati ya tatu tofauti zilizotolewa na kutajwa kuwa gharama halisi ya ujenzi wa miundombinu kwenye mpango wa Zanzibar kushiriki kama sehemu ya muandaaji wa Fainali zsa Kombe la Mataifa ya Afrika {AFCON} mwakani. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Hii inatokana ya mgongano wa takwimu zinazohusu gharama ya utekelezaji mradi ambao serikali imeubuni utakaohusisha ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo, viwanja viwili vidogo vya mazoezi, hoteli kwa ajili ya kambi ya timu shiriki pamoja na barabara ya njia sita inayotoka makutano ya Maungani hadi Fumba kunakojengwa kiitwacho Kijiji cha AFCON 2027.
Inavyojulikana, mpaka Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi alipotaja takwimu tofauti akiashiria kupingana na aloitoa makamu wa kwanza wa rais mstaafu Othman Masoud Othman, hivi karibuni, gharama ya mradi huo kama ilivyotajwa na Waziri wa Fedha Zanzibar, Dk. Juma Malik Akili, ni Sh. 1.69 Trilioni.
Waziri huyo alitaja kiwango hicho mnamo tarehe 11 Juni 2026, mbele ya Baraza la Wawakilishi katika hotuba yake akiwasilisha smakadirio na mapato na matumizi ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.
Hata hivyo, waziri huyo, kwenye taarifa yake mpya ya juzi, kupitia kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC-TV}, alisikika akitoa maelezo yanayozua utata kuhusu gharama halisi za mradi huo. ZBC ilimnukuua akisema taarifa ya Sh. 1.69 Trilioni aloizungumza katika baraza la wawakilishi, tarehe 11 Juni, si sahihi.
ZBC imesema {Waziri Dk. Akili} amenukuliwa vibaya au {itakuwa} video mjongeo inayoonekana kwenye mtandao wa YouTube imechezewa. Badala yake, sasa waziri huyo anataja Sh. 1.069 Trilioni kuwa ndio kiwango sahihi.
Ndio hapa Mnadhimu wa Wawakilishi wa ACT Wazalendo, Profesa Omar Fakih Hamad, akisongoza wajumbe wenzake, anataka serikali itoke upya na kutoa ufafanuzi wa lipi la kulishika kuwa ndio sahihi.
Prof. Fakih katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Ofisi Kuu ya chama Vuga, anasema wameshtushwa na kauli za “kubabaisha za Serikali kuhusu ukweli na usahihi wa gharama za ujenzi wa miundombinu ya AFCON 2027 Zanzibar.”
Tanzania ni miongoni mwa mataifa matatu yaliyopewa hadhi ya uenyeji wa mashindano hayo.
“Tunaitaka Serikali kutowababaisha wananchi na kutoa taarifa sahihi na kamilifu kwa umma na kuweka wazi juu ya tofauti zilizojitokeza katika taarifa za gharama za ujenzi wa miundombinu inayohusiana na maandalizi ya Kombe la AFCON 2027,” anasema.
Utata wa ukweli na usahihi wa gharama halisi za maandalizi ya mashindano hayo, umetokana na aliyoyaeleza Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, aliyehoji ni kwa namna gani Sserikali itamudu kuulipa mkopo iliyoupata kutoka benki ya kibiashara kwa ajili ya kukidhi gharama za maandalizi hayo.
Akizungumza kwenye mahojiano na Muandishi na Mtangazaji Charles William wa kituo cha televisheni cha Wasafi TV cha jijini Dar es Salaam, Othman alitaja gharama za mradi wa AFCON2027 kuawa ni Sh. 1.69 Trilioni, akisema haoni busara ya serikali kufikia kujiamini kukopa kiasi chote hicho ili kutekelezea mradi ambao haoni kama ulikuwa lazima.
Hatua hiyo ndiyo ilimuibua Dk. Mwinyi ambaye alipokuwa akizindua huduma ya usafiri wa umma kutumia mabasi yanayotumia nishati ya umeme, alisema gharama halisi za mradi huo ni Dola za Marekani 150 milioni – sawa na kiasi cha Sh. 300 Bilioni.
Dk. Mwinyi aliyekuwa akizungumza kwa ujasiri akitumia lugha ya picha, alisema, “kwa wale wasojua, gharama za mradi wa kijiji cha michezo cha AFCON2027 ni Dola 150 milioni tu kiasi cha Sh. 300 Bilioni na sio kwa kujenga uwanja wa kisasa wa kuchezea, kutakuwa na viwanja vidogo viwili vya mazoezi, hoteli na mambo mengine ya kuwezesha mashindano kufanyika Zanzibar.”
Kauli hiyo ikachochea hisia kali. Kundi la wawakilishi wa ACT Wazalendo likiongozwa na Prof. Fakih likatoka hadharani: “Tumepata wasiwasi mkubwa wa tofauti ya gharama halisi zilizotolewa na serikali moja. Taarifa ya kwanza ya Waziri wa Fedha ndani ya Baraza la Wawakilishi… ya pili ile iliyotolewa na Rais, mkuu wa nchi… taarifa ya tatu iliyotolewa tena na Waziri wa Fedha {ambayo} inapingana sana na taarifa yake ya kwanza aliyoitoa katika Baraza la Wawakilishi.”
Barazani Waziri Dk. Akili alisema kufuatia fursa ya kuwepo mashindano ya AFCON 2027, “Serikali imetenga kiasi cha Sh. 1.69 Trilioni ili kuwekeza katika kuimarisha maandalizi ya kitaifa katika miundombinu ya michezo, usafiri, utalii na huduma za kijamii kwa lengo la kutumia mashindano hayo kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi, ajira na kulitangaza taifa kimataifa.”
Fainali za AFCON zinaandaliwa kwa utatu – Tanzania, Kenya na Uganda. Serikali ya Tanzania imesema mashindano yatafanyikia viwanja vya Benjamin Mkapa, Azam Complex Chamanzi, Meja Jenerali Isamuyo vya Dar es Salaam, Sheikh Amri Abeid Arusha na Jamhuri Dodoma.
Shirikisho la Kandanda Tanzania {TFF} lenye jukumu mahsusi katika utekelezaji wa maandalizi ya mashindano hayo, limeipatia Zanzibar nafasi ya kuwa sehemu ya maandalizi.