MAKABIDHIANO rasmi ya ofisi ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Dar es Salaam yamefanyika leo, ambapo aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omar, amekabidhi rasmi ofisi kwa Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Abbas Ramadhani.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika katika ofisi za Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufuata taratibu za kiutawala za taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mabadiliko ya uongozi yaliyotangazwa na Bakwata.
Akizungumza baada ya makabidhiano, Sheikh Abbas Ramadhani ameahidi kushirikiana na viongozi, watumishi na waumini katika kuendeleza shughuli za Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam na kusema kuwa yeye na shekhe walid taratibu zao za kimaisha ziko palepale na kuahidi kwenda kumuona mara kwa mara kuomba ushauri wa kuendeleza ulezi wa kulea roho za watu huku akisema uteuzi huo ameupokea kwa huzuni kwa kutafakari kwa kina juu ya nafasi hiyo.
Kwa upande wake, Sheikh Walid Alhad Omar ameomba watu kumpa ushirikiano sheikh Abbas katika kuiongoza taasisi hiyo ya dini mkoa wa Dar es salaam.
Katika makabidhiano hayo, nyaraka mbalimbali za kiutawala, mali za ofisi pamoja na majukumu ya uongozi yalikabidhiwa rasmi kwa kaimu Sheikh wa Mkoa, ambaye sasa atasimamia shughuli za ofisi hiyo kwa kipindi cha ukasimu.