KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani, Benjamini Ntele, amesema kuwa mtu aliyemtuhumu Makamu mwenyekiti wa chama hicho (Tanzania Bara), John Heche, siyo mwanachama wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, tarehe 17 Julai 2026, Ntele amesema, “…kuna watu wanatumia kofia ya Chadema, kukichafua chama hicho.”
Ntele amesema, mtu huyo amekuwa akiitambulisha kwa wananchi kuwa mwanachama wa Chadema, wakati ukweli ni kwamba siyo mwanachama wake.
“Pale Kibaha, mkoani Pwani, kuna mtu anaitwa Mohemed Ngozi, mwanachaam wa NCCR- Mageuzi. Huyu bwana mwaka 2025, alikuwa mgombea udiwani wa NCCR-Mageuzi, katika halmashauri ya Kibaha Vijijini.
“Jana ameitisha mkutano na waandishi wa habari na akajitambulisha kuwa anaitwa Shaban Ally Mchezo, mwenyekiti wa Chadema, jimbo la Kibaha. Akatumia nafasi hiyo, kumchafua na kumshambulia makamu mwenyekiti wetu,” amefafanua.
Kwa takribani wiki moja sasa, kumeibuka watu mbalimbali, wanaodai kuwa wanachama na viongozi wa Chadema, wakiripotiwa kumtuhumu Heche kuwa anatumia vibaya michango ya wadau na kutaka achunguzwe.
Aidha, kupatikana kwa taarifa hizi, kumekuja siku moja baada ya gazeti dada la MwanaHALISI, kuripoti kuwapo mtandao mpana wa watu, unaofadhiliwa na wabaya wa Chadema, kulipa watu kuita waandishi wa habari, ili kumchafua na kumvunjia heshima Heche.
Miongoni mwa wanaotajwa watumika kulipa ili kuvuruga Chadema, ni pamoja na Emmanuel Masonga, aliyewahi kuwa Katibu wa Chadema Kanda ya Kati.
Masonga alikuwa mmoja wa wanatimu ya Freeman Mbowe, kwenye uchaguzi mkuu wa 21 Januari mwaka jana na bado mpaka sasa hajapona.
Katibu huyo wa zamani wa Chadema, ndiye anayetumiwa na watu wa mfumo, kutapakanya mamilioni ya shilingi, ili kudhoofisha chama hicho, kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari, kumshambulia Heche. Masonga amekana madai hayo.
Aliyemtaja Masonga kuwa “kuwadi,” ni aliyekuwa katibu wa Kanda ya Pwani, Jerry Kerenge, anayesema ameambiwa na Masonga kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kumchafua Heche na kwamba atalipwa kiasi cha Sh. 2 milioni.
Mwingine anayetajwa kwenye mradi huo, ni Charles Odero, aliyefukuzwa uanachama wa chama hicho na sasa amejipachika uenyekiti wa anachoita, “Kamati ya Maridhiano ya Kitaifa.”
Ntele amesema, wale waliokuwa wameandaa kile alichokiita mtego dhidi ya chama hicho, hatimaye wameingia kwenye 18 za wanachama wa Chadema Kanda ya Pwani.
Ntale amemtaja mwenyekiti halali wa jimbo la Kibaha Vijijini, kuwa ni Shaban Ally na ambaye alikuwapo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, uliofanyika makao makuu ya Kanda ya Pwani, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Mchezo aliwaambia waandishi wa habari kuwa amekuwa akishawishiwa mara kwa mara, kihujumu chama hicho, lakini amekataa.
Alisema, “Niliitwa Magomeni na kuahidiwa kupewa Sh. 1 milioni na mtu aliyewahi kuwa mwanachama wa chama hicho Kanda ya Pwani.”
Anasema, baada ya kushindwa kumshawishi kuhujumu chama, kulijitokeza mtu mwingine akitumia jina lake na kujitambulisha kuwa mwenyekiti wa Chadema, Jimbo la Kibaha Vijijini.
Akaonya dhidi ya matumizi ya jina lake na kusisitiza kuwa yeye ndiye kiongozi rasmi katika eneo hilo na kamwe hatakubali kuona Chadema inahujumiwa.
Anasema, alijiunga na Chadema mwaka 2015 na hivyo hawezi kushiriki kwenye dhambi ya usaliti. Amezitaka mamlaka husika kuwabaini na kuwachukulia hatua watu wote wanaohusika na tukio hilo.
Mbali na wanaotumia kofia ya Chadema, baadhi ya wanachama wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), wakiongozwa na Benson Kigaila, katibu wake mkuu, nao wamekuwa wakitumiwa kumsakama Heche.