CHAMA cha ACT-Wazalendo na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, “wamefunga makubaliano mengine ya kisiasa visiwani humo.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Mkataba wa makubaliano unaolenga kuimarisha ushirikiano na kutafuta suluhisho la kudumu la tofauti za kisiasa Visiwani zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, umesainiwa Ikulu mjijni Unguja leo Alhamisi, tarehe 9 Julai 2026.
Waraka wa pamoja wa makubaliano yaliyolenga kunasua Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), umesainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Mohamed Said Dimwa na naibu katibu mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Sheha.
Mazungumzo yalianza Novemba 2025 na kuongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi. Yalisimamiwa na marais wawili wastaafu Visiwani, Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein.
Wengine walioshiriki mchakato wa maridhiano, ni Othman Masoud, mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji, mwenyekiti mstaafu wa chama hicho na Omar Said Shaban, mwanasheria mkuu wa ACT -Wazalendo.
Mazungumzo yalikuja kufuatia chama cha ACT- Wazalendo, kugoma kutambua matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais wa Zanzibar, kwa madai kwamba uchaguzi uliokiingiza madarakani CCM, ulitawaliwa ghiliba na wizi wa kura.
Aidha, hatua hiyo inakuja baada ya takriban miezi sita ya kutokuwepo kwa makubaliano kati ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo – vyama viwili vikuu vinavyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani, kwa mujibu wa Katiba.
Katiba ya sasa ya Zanzibar, inayotambua kuwapo kwa muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa na ambayo sasa itafumuliwa na kuandikwa upya, ilipitishwa mwaka 2010. SUKI imetajwa katika Ibara ya 9 (3) ya Katiba hiyo.
Waraka wa makubaliano uliwasilishwa na Katibu wa Kamati ya Maridhiano ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi (BLM), Mansura Mosi Kassim.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha waraka huo, Mansura alisema mchakato huo ulianza kupitia vikao tisa vilivyofanyika kuanzia 9 Novemba mwaka jana, huku kamati ndogo nazo zikifanya kazi ya kuchambua hoja mbalimbali na kuwasilisha mapendekezo yaliyowezesha kufikiwa kwa makubaliano.
Alisema, vikao viwili vya mwisho vilifanyika Ikulu Zanzibar chini ya uongozi wa pande hizo mbili na baadaye kufanikisha kukamilika kwa hatua ya awali ya mazungumzo hayo.
Kwa mujibu wa waraka huo, pande hizo mbili zimekubaliana mambo saba ya msingi yatakayoongoza mchakato wa maridhiano.
Miongoni mwa makubaliano hayo ni kuimarisha ushirikiano kutokana na mazingira ya Zanzibar, kuchukua hatua stahiki katika kutekeleza makubaliano, kuhakikisha mchakato unakuwa shirikishi kadri itakavyohitajika na mchakato huo, kuongozwa na misingi ya ukweli na kutanguliza maslahi ya Zanzibar.
Mengine yaliyofikiwa, ni kutekeleza ajenda zilizokubaliwa hatua kwa hatua na kuanza utekelezaji wa makubaliano mara moja, pamoja na kuendelea kushirikiana hadi kupatikane suluhisho la kudumu.
Hatua hiyo inatajwa kuwa mwanzo wa awamu mpya ya maridhiano ya kisiasa inayotarajiwa kuimarisha umoja, utulivu na maendeleo ya Zanzibar.