MSANII maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Rajabu Ibrahim, maarufu kama Harmonise, anatarajiwa kuwa mmoja wa washiriki wa mbio za Pande Msakuzi Marathon, zitazofanyika ndani ya Hifadhi ya Pande Agosti Mosi mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Harmonise ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Uhifadhi Wanyamapori Tanzania (TAWA), Vicky Kamata kumualika msanii huyo kushiriki mbio hizo maarufu nchini.
Kamata amesema kwa kuwa Harmonise ni ‘Tembo na Tembo’ wanasimamiwa na TAWA, ni jambo njema sana kwa msanii huyo kuja kutoa burudani ndani ya hifadhi hiyo iliyopo wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Mwanamuziki huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa yuko tayari kushiriki mbio hizo na kutoa burudani siku hiyo kama sehemu ya kutangaza utalii wa Pande.

Amesema anafanya mawasiliano na waandaji wa mbio hizo, Msakuzi Sports Promotion na TAWA ili aweze kushiriki siku hiyo huku akiahidi burudani ya aina yake.
Akizungumzia maandalizi ya mbio hizo, Mwenyekiti wa Msakuzi Sports Promotion, Dk. John Kisimbi amesema kila kitu kinaenda vizuri na amewasihi wananchi kutoka sehemu mbalimbali nchini kuendelea kujisajili kupitia www.pandemarathon.store.tz kwa kulipia shilingi 35,000 tu.
Kwa mujibu wa Dk. Kisimbi, mgeni rasmi siku hiyo anarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki ambaye pia Mbunge wa jimbo la Kibamba.
Dk. Kisimbi ambaye amesisitiza kuwa mbio hizo ni za aina yake amesema ‘KITI’ zinapatikana Sabasaba kwenye Banda la Maliasili na Utalii.

“Kauli mbiu ya mwaka huu ni Afya na Utalii, tunakimbia ndani ya hifadhi ya Pande, anga lote ni kijani, unakimbia unaona wanyama wa kila aina. Hizi ni mbio za kipekee kabisa,” anasema Kisimbi
Mmoja wa Waratibu wa mbio hizo, Chester Kapinga, amesema Pande Marathon ni zaidi ya mbio kwani baada ya kukimbia kuna ‘bata’ la kutosha.
“Tumeandaa burudani za muziki wa dansi, nyama choma za wanyamapori, vinywaji vya aina zote. Huo ni mtoko wa aina yake, usipange kukosa,” alisema Kapinga.