MKAZI wa Sirorisimba-Butiama, Chacha Marwa Chacha (27), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza leo 16 Juni 2026, kwa tuhuma za kulawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 9 (jina limehifadhiwa kwa sababu za kisheria). Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
​Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Christian Mwalimu, Wakili wa Serikali Clara Muhando ameieleza mahakama kuwa tukio hilo lilitokea tarehe isiyofahamika mwezi Septemba 2025 katika eneo la Isanzu, Shule ya Godbless Pre and Primary School, Kata ya Bugogwa jijini humo, ambapo mshtakiwa anadaiwa kutenda kitendo hicho cha ukatili dhidi ya mtoto huyo.
​Katika kesi hiyo ya jinai yenye namba 13435/2026, mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la kulawiti, kinyume na Kifungu cha 154(1)(a)(2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023.
​Hata hivyo, mshtakiwa amekana shtaka hilo. Hakimu Mwalimu anayesikiliza kesi hiyo ameeleza kuwa kosa hilo linadhaminika kwa masharti, ikiwemo kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho halali vya taifa, barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa na kila mdhamini kusaini hati ya dhamana ya Shilingi milioni tatu.
​Mshtakiwa ameshindwa kukidhi masharti ya dhamana kwa kuwa hakuwa na mdhamini wa pili, hivyo amerejeshwa rumande hadi 30 Juni 2026, kesi hiyo itakapoitwa kwa ajili ya kusomewa hoja za awali na usikilizwaji.